Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu(OWM-KVAU) katika mwaka 2023/24 imepanga kutekeleza mambo matano ikiwamo kuwezesha na kuratibu masuala ya ukuzaji wa fursa za ajira na kazi za staha.
Aidha, imepanga kuwawezesha watu wenye ulemavu kujiajiri na kuajiriwa kwa kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi na marekebisho kutoka watu 460 hadi 1,400.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameyasema hayo Aprili 5, 2023 bungeni alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
Amesema masuala hayo yatafanywa kwa kuboresha na kutekeleza sera, mikakati na mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata fursa za kujiajiri au kuajiriwa ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Pia, amesema kwa mwaka huo serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria za kazi, uratibu wa ajira za wageni na masuala yote yanayohusu usalama na afya mahali pa kazi.
Kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii, Majaliwa amesema katika mwaka 2023/24, Serikali itaendelea kuimarisha sekta hiyo kwa kuhakikisha wananchi wengi wanajumuishwa katika mpango wa hifadhi ya jamii wa uchangiaji.
"Natoa wito kwa sekta isiyo rasmi ikiwemo mama/baba lishe, machinga, bodaboda, wakulima, wavuvi, wafugaji, na wengineo kujiunga na mifuko hiyo kwa manufaa yao ya baadaye,"amesema.
Kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mhe.Majaliwa amesema itaendelea kuimarisha uwezo wa mfuko huo katika kutoa mikopo na mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wengi ili kuwawezesha kujiajiri na kuchangia uchumi wa Taifa.
Vilevile, amesema itaanzisha kampeni ya kuwashawishi vijana kushiriki katika kilimo.