Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHANGO WA SEKTA YA MADINI KWENYE PATO LA TAIFA WAZIDI KUONGEZEKA





Na Mwandishi wetu,TABORA.

IMEELEZWA kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita mchango wa Sekta ya Madini umeendelea kukua  hadi kufikia asilimia tisa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachimbaji wadogo  wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu Wilayani  Nzega mkoani Tabora kupitia mahojiano maalum wamesema kuwa mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa Serikali kupitia Tume ya Madini  wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea  kuongezeka kwa uzalishaji wa madini unaofanywa na wachimbaji wadogo kwa kutumia  teknolojia za kisasa.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo wa eneo hilo, Peter Mashiri, kutoka Kikundi cha  Msilale kilichopo katika eneo hilo  amesema kuwa kuongezeka kwa mapato yatokanayo na Sekta ya Madini kumetokana na matumizi ya teknolojia za kisasa na jitihada za Serikali za kuhakikisha makundi yote yanashiriki katika sekta hiyo.

Akizungumzia manufaa ya kikundi hicho kwa jamii inayouzunguka mgodi wake Mashiri amesema kuwa kikundi cha Msilale kimesaidia kutoa ajira kwa vijana wanaozunguka mgodi ambapo hadi sasa watu zaidi ya 48 wameajiriwa.

“Tunaipongeza Serikali kwa namna inavyowajali wachimbaji wadogo kwa kutoa leseni  kwa makundi hayo ambayo imesaidia kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, tunaiomba Serikali iendelee kuwagawia maeneo ambayo bado yanamilikiwa na wachimbaji wakubwa bila kuendelezwa.

Kwa upande wa Katibu wa kikundi hicho, Magreth Emmanuel amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Sekta ya Madini kwa kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi.

Ameongeza kuwa uwepo wa Sekta ya Madini umefungua fursa na hamasa kwa wanawake wengi ambao kwa sasa wameanza kujihusisha na shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, na biashara ya madini sambamba na kutoa huduma kwenye migodi ya madini na kujipatia fedha kwa ajili ya kujikimu na kuhudumia familia zao.

Naye Msimamizi wa Mazingira wa kikundi hicho amesitiza kuwa mgodi huo umeendelea kuboresha mazingira yake kwa kuweka mitambo ya kisasa ambayo inawasaidia kuingia na kutoka ndani ya migodi, tofauti na awali ambapo walikuwa wanatumia kamba kushuka chini jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa usalama wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com