Dotto Kwilasa, DODOMA.
SERIKALI imewatoa hofu wananchi kuhusu mijadala inayoendelea nchini inayotokana na ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG)na kueleza kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi bila woga wowote ili kulinda rasilimali za watanzania.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa amesema hayo leo Aprili 19,2023 Jijini Dodoma kwenye hafla baina na Waandishi wa habari iliyoambatana na Iftar ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Msigwa amewata wananchi kuachana na mijadala ya ripoti hiyo ambayo imejaa upotoshaji na isiyojenga yenye lengo la kuharibu taswira ya nchi na badala yake wajikite kwenye ujenzi wa Taifa .
"Niwatoe hofu wananchi, ripoti ya CAG ni nyenzo inayotumiwa na Serikali kusimamia rasilimali za watanzania,hivyo niwahakikishie kupitia ripoti hiyo Serikali ipo macho kulinda na kutetea rasilimali,achaneni na taarifa za mitandaoni zinazokatisha tamaa,"amesema.
Kuhusu miradi ya kimkakati Msigwa amesema mwendo ni uleule hakuna kilichobadilika wala kusimama na kutolea mfano mradi wa reli Morogoro -Makutopora kuwa unaendelea kutekelezwa ukiwa umefikia asilimia 93.3.
"Miradi yote ya kimkakati inaendelea kutekelezwa, Serikali ya Rais Samia Ina nia ya dhati na itahakikisha mipango yote inatekelezwa ikiwemo mabehewa ya ghorofa,mradi wa uzio wa Tembo ambao umeanza Kwa mara ya kwanza nchini na barabara ya mzungu ya Dodoma ambayo imefikia asilimia 18.
Kama ilivyo kwa Viongozi wengine katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan,Msemaji huyo wa Serikali pia ametumia nafasi hiyo kuwataka Waandishi wa habari na watanzania kwa ujumla kuendelea kutendeana mema na kuepuka chuki na majungu miongoni mwao.
"Kiu yangu kila siku ni kuona mnashirikiana,mnapendana na kusaidiana,tukiishi Kwa upendo tunakuwa na utulivu unaotufanya tuwe na bidii Katika ujenzi wa Taifa lefu,tuheshimiane siku zote kwa kuzingatia miiko na maadili ya nchi yetu,"amesisitiza Msigwa.