Mgeni Rasmi katika mahafali ya 13 shule ya Sekondari Isimila iliyopo Mkoani Iringa Bw. Masozi Nyirenda (wa pili kutoka kulia) akiingia ukumbini na msafara wa wahitimu. Kulia ni Mkuu wa Shule Bw. Frank Mahenge na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Dkt. Nasra Habib.
Mgeni Rasmi Masozi Nyirenda (kulia) na Mkuu wa shule Frank Mahenge (kushoto) wakifurahia burudani kutoka kwa wahitimu (hawapo kwenye picha) katika sherehe za mahafali ya 13 ya kidato cha sita shule ya Sekondari Isimila iliyopo mkoani Iringa.
Mgeni Rasmi Masozi Nyirenda (katikati) akipokea nakala ya risala kutoka kwa wahitimu wakati wa mahafali ya 13 ya kidato cha sita shule ya Sekondari Isimila mkoani Iringa. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule Dkt. Nasra Habib na kushoto ni Mkuu wa Shule Frank Mahenge.
Wahitimu wakidato cha Sita wakisoma risala mbele ya Mgeni Rasmi (hayupo pichani) katika sherehe za mahafali ya 13 ya kidato cha sita shule ya sekondari Isimila mkoani Iringa.
Mkuu wa Shule Bw. Frank Mahenge akielezea historia ya shule wakati wa mahafali ya 13 ya kidato cha sita shule ya Sekondari Isimila Mkoani Iringa. Waliokaa ni Mgeni Rasmi Masozi Nyirenda na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Dkt. Nasra Habib.
Mgeni Rasmi Bw. Masozi Nyirenda akisisitiza jambo katika sherehe za mahafali ya 13 ya kidato cha sita shule ya Sekondari Isimila Mkoani Iringa. Waliokaa ni Mkuu wa shule Frank Mahenge na mdau wa shule Dkt. Ave Maria Semakafu.
Mgeni Rasmi Masozi Nyirenda akitoa vyeti kwa wahitimu wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Isimila mkoani Iringa katika mahafali ya 13 shuleni hapo.
*************************
Na MWANDISHI WETU.
WANAFUNZI wengi wanaomaliza masomo yao ya Sekondari na kufanya vizuri sababu imetajwa kuwa ni bidii ya kujituma katika kufikia ndoto zao lakini pia nidhamu ya kujali muda na kusimamia malengo waliyojiwekea kwenye masomo yao.
Hayo yametajwa katika sherehe za mahafali ya 13 ya kidato cha sita Shule ya Sekondari Isimila mkoani Iringa wakati wa hafla iliyofanyika jana shuleni hapo ambapo mgeni rasmi alikuwa Meneja Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bw. Masozi Nyirenda akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo.
Awali akielezea historia ya shule hiyo Mkuu wa shule Bw. Frank Mahenge alisema, shule ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita na jumla ya wanafunzi 1,178 wasichana wakiwa ni 835 na wavulana 343 huku kidato cha tano na sita wakiwa ni wasichana pekee.
Amesema, shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kwenye mitihani ya mwisho ya Taifa na kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo 2020 - 2022 shule imekuwa ikifaulisha kwa asilimia 100 daraja la kwanza hadi la tatu hivyo kuwafanya wanafunzi wengi kutamani kusoma katika shule hiyo.
"Shule yetu inafanya vizuri kwenye matokeo ya mwisho hivyo kuvutia wanafunzi kuomba nafasi za kujiunga na hii imepelekea tuwe na upungufu wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kama vile mashine ya kurudufu, maktaba kwa ajili ya kujisomea, jengo la utawala, nyumba za walimu pamoja na bwalo, alisema Mahenge’’
Nao wahitimu wa kidato cha Sita katika risala yao walisema, wanajivunia kuwa sehemu ya familia ya shule ya sekondari Isimila kutokana na misingi, mikakati na malengo ya shule hiyo ambayo inawawezesha kufanya vizuri na kuifanya shule hiyo kuwa bora.
Mgeni Rasmi katika mahafali hayo Bw. Masozi Nyirenda Meneja Miradi kutoka TEA alisema, inafurahisha kuona kuwa shule ya Sekondari Isimila ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri ambapo matokeo ya miaka mitatu yameonesha hakuna aliyepata ufaulu wa daraja sifuri. Nidhamu na bidii ya masomo imesaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho.
“Nimefurahishwa kuona namna uongozi wa shule hii unavyoendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wake wanaendelea kupata matokeo mazuri. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa vinne, Ofisi mbili lakini pia kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri kutengeneza madawati 130, amesema Nyirenda”
Nyirenda alisema, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilianzishwa kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unalenga kusaidia jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa Elimu bora na kwa usawa hapa nchini. Kupitia Mfuko huo wa Elimu wa Taifa, ufadhili wa miradi ya Elimu yenye thamani ya Bilioni 1.1 katika Mkoa wa Iringa umetolewa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015/2016 hadi 2022/2023
Aidha, aliushauri uongozi wa shule kuwasilisha maombi ya ufadhili kwenye Ofisi za Mamlaka kwa ajili ya upungufu wa miundombinu ili maombi hayo yaweze kufikiriwa kadri ya upatikanaji wa fedha, lakini pia kutumia michango ya wadau wa Elimu ndani ya Halmashauri kwani inaweza kusaidia kupunguza changamoto hizo.
Aliwapongeza wahitimu wote wa kidato cha sita kwa hatua waliyofikia na kuwakumbusha kuwa, mafanikio hayaji pasipo maandalizi hivyo anaamini wamejiandaa vya kutosha na wako tayari kwa mitihani yao ya mwisho ili waweze kuendelea na ngazi nyingine ya Elimu baada ya kuhitimu.
Social Plugin