Mwanafunzi wa UDSM Samora Mathayo akionesha mkojo wa binadamu ambao umefanyiwa utafiti na kuonesha kuwa unafaa kwa kilimo.
Mwanafunzi wa UDSM, David Zunda akionesha bidhaa zilizotengenezwa kwa magamba ya samaki.
Mwanafunzi wa UDSM David Zunda akimuelezea Mkuu wa Ndaki ya CoNAS Profesa Flora Magige namna alifanya utafiti na kubaini magamba ya samaki yanavyoweza kutengeza bidhaa .
Mkuu wa Ndaki ya CoNAS Profesa Flora Magige akipita kwenye moja ya banda ambalo linaonesha utafiti wa kisayansi uliofanywa na wanafunzi na walimu wa Ndaki hiyo .
***********************
Na Mwandishi Wetu
NDAKI ya Sayansi Asili na Sayansi Tumizi (CoNAS), ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imesema walimu na wanafunzi wa ndaki hiyo wataendelea kufanya utafiti ambao unaenda kukuza uchumi na kumkomboa mwananchi wa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Ndaki hiyo, Profesa Flora Magige wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwenye maonesho ya wiki ya utafiti UDSM iliyoanza Aprili 11 hadi 13, 2023.
Prof. Magige amesema CoNAS inahusisha idara sita ambazo ni Kemia, Fizikia, Biolojia, Botanyi, Hisabati na Zoologia, ambapo wahadhiri na wanafunzi wamekuwa wakifanya utafiti kila mwaka ambao unawaongezea ujuzi wa namna ya kusaidia jamii.
Amesema wahadhiri na wanafunzi wa CoNAS wamekuwa wakifanya utafiti wenye kuongeza thamani ya mazao ambayo yanasaidia viwanda kuweza kuzalisha jambo ambalo matokeo yake yatachangia ajira na kukuza uchumi.
“Haya ni maonesho ya utafiti ambao umefanywa na UDSM kupitia ndaki zake mbalimbali ikiwemo yetu ya CoNAS, ambapo kupitia matokeo haya ya utafiti tumeweza kutatua changamoto katika jamii kama afya, uchumi na nyingine,” amesema.
Mkuu huyo wa Ndaki amesema pia wameweza kuongeza ubora katika bidhaa za viwanda katika eneo la virutubisho, wamefanya utafiti wa dawa za binadamu na mbolea ambazo zinatumika katika kilimo, hivyo wanaamini watainua sekta hiyo.
Mratibu wa Utafiti na Uchapishaji CoNAS, Dk Steven Nyandoro alisema wiki hiyo imekuwa ikiwasaidia wahadhiri na wanafunzi kuanzia shahada ya kwanza, ya pili na tatu kuja na majibu ya changamoto zinazokabiliana na jamii.
Dk. Nyandoro amesema utafiti unaofanywa na idara mbalimbali UDSM umekuwa ukifanyika kwa kushindanishwa kwa miaka nane sasa, ambapo baadae wanapatikana washindi ambao wanawakilisha chuo katika maonesho mbalimbali kama Sabasaba na Nanenane.
Amesema CoNAS imefanya utafiti wa kutafuta dawa dhidi ya magonjwa sugu kama malaria ambapo wamegundua mmea unaopatikana wilayani Kilwa mkoani Lindi ambao unaweza kupambana na magonjwa hayo.
“Utafiti unaofanywa ndani ya Ndaki yetu, umekuwa wenye kutatua changamoto kwa jamii, lakini lazima tushindanishwe ili kupata mshindi, mfano kwa sasa vijana wetu wamefanya utafiti ambao unatumia magamba ya samaki ambayo yamefanywa kuwa bidhaa na sio takataka tena.
Pia kuna watafiti wamegundua kuwa mkojo wa binadamu ni mbolea nzuri, panya wanavyosababisha magonjwa na mengine mengi ambayo yanatatua changamoto za jamii,” amesema.
Kwa upande wao wanafunzi wa UDSM, Samora Mathayo aliyefanya utafiti wa matumizi ya mkojo wa binadamu kama mbolea na David Zunda aliyefanya utafiti wa matumizi ya magamba ya samaki wamesema wanachofanya ni matokeo ya elimu bora wanayopewa na walimu wao.
Wanafunzi hao wameiomba Serikali na wadau wengine kuwapatia mtaji ili waweze kuendeleza ubunifu wao na kuwezesha kuajiri vijana wakitanzania.
Wamesema changamoto ya ajira ambayo inakabili nchi na dunia kwa ujumla inaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuwezesha wabunifu.
Social Plugin