Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Kilumbe Ng'enda ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna inavyoshoghulikia changamoto ya ajira kwa vijana nchini kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo imekuwa chachu ya vijana kujiajiri na kuajiri wenzao.
Akichangia Aprili 6, 2023 bungeni mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Mbunge huyo amesema programu hiyo iwe endelevu kwa kuwa ina manufaa yenye tija kwa nguvukazi ya Taifa kupata ujuzi unaowawezesha kujiajiri sambamba na kujikwamua kiuchumi.
"Nimetembelea Chuo cha VETA Kigoma nimeshuhudia kijana ameweza kutengeneza redio na anarusha matangazo mwenyewe katika jamii inayomzunguka, hivyo kijana huyo akiendelezwa anaweza kufanya mambo makubwa sana," amesema.
Vilevile, amesema uwepo utaratibu wa kuwawezesha vitendea kazi vijana hao wanapomaliza mafunzo yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Pia, ameshauri serikali kuweka utaratibu maalum wa kuendeleza vipaji vya vijana wabunifu ambao wamenufaika na programu hiyo.
Social Plugin