Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MANKA ANUSURIKA KIFO KWA KUCHAPWA VIBOKO KWA ZAMU NA SUNGUSUNGU TUHUMA ZA KUIBA PESA ZA MTEJA GESTI



Muonekano wa majeraha katika mwili wa Manka


Na Suzy Luhende -Shinyanga, 

Mwanamke aitwaye Manka Mushi (26) mfanyakazi wa baa na nyumba ya kulala wageni mkazi wa Kijiji cha Ikoma Kata ya Itilima Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga amenusurika kifo baada ya kuchapwa viboko hadharani na jeshi la jadi sungusungu baada ya kutuhumiwa kuiba Shilingi 420,000/= za mteja wake.


Inaelezwa kuwa mwanamke huyo ambaye sasa amelazwa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu alikutwa na mkasa huo Aprili 14,2023 katika kijiji cha Ikoma.

Manka anasema wakati akiendelea kufanya kazi baa na nyumba ya kulala wageni katika kijiji hicho ndipo mwanaume aitwaye Julias Marimo ambaye alikuwa akimtaka kimapenzi na kumkataa alimuomba ampelekee shuka chumbani.

Manka akisimulia mkasa huo uliomkuta amesema ilikuwa majira ya saa sita usiku alipopeleka shuka baada ya mteja kuomba, ndipo alimkaba koo akimtaka kurudisha fedha ambazo anahisi alichukua alikataa kuhusika na wizi huo na kumwambia kwa kuwa alimkataa atamtambua na alianza kupiga kelele za kuomba msaada na kufanikiwa kutoka ndani.

"Usiku huo huo mteja alikuja kugonga tulipokuwa akaomba shuka niliinuka kumpelekea, lakini cha kusikitisha baada ya kufikisha shuka alinigeuka akasema nimeiba hela alinipiga sana akiniambia kwa nini nilimkataa atanionyesha mimi nani nilimwambia sijachukua hela na asubuhi akaenda kwa kamanda wa sungusungu wa Kijiji nikaitwa”, ameeleza Manka.

"Kufuatia hatua hiyo niliambiwa na kamanda wa sungusungu twende uwanjani na baada ya kufika nilikuwa mwanamke peke yangu nikaambiwa nilale chini katikati ya wanaume zaidi ya 30 ukaletwa mzigo wa fimbo wakaanza kunipiga viboko kwa zamu nikijaribu kuinuka wengine wanapiga mgongoni na kichwani", amesema.

Amesema aliwapa namba ya mama yake mzazi ambaye anaishi Jijini Arusha walimpigia na kuzungumza naye kisha kumtaka atume hela lakini aliwaomba wampeleke polisi, na baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya walimpeleka ofisi ya Kata kwa ajili ya kutoa maelezo, lakini walikataa kumpokea.

Amesema anamshukuru Mungu kwa sasa anaendelea vizuri tofauti na awali, ambapo sehemu ya makalio na mgongoni kulikuwa kumejaa vidonda ambapo ameiomba serikali kuchukua hatua kali kwa sungusungu waliomfanyia kitendo hicho.

Kwa upande wake mhudumu wa wodi namba saba ya wanawake na upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Weru Kiula amesema walimpokea mwanamke huyo April 14 mwaka huu akiwa na hali mbaya ana vidonda kwenye makalio na mgongoni lakini kwa sasa anaendelea vizuri.

Afisa ustawi wa jamii hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Prisila Mushi amesema matukio ya wanawake kupigwa na sungusungu yamekuwa yakitokea mara kwa mara na ameiomba serikali kuchukua hatua kali kwa watu waliohusika na ukatili huo.

Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba wanawatafuta watu wote waliohusika na kumpiga viboko mwanamke huyo ambao walikimbia baada ya kufanya tukio hilo.

" Kweli tukio hili lipo na waliofanya tukio hili la kumpiga viboko mwanamke huyu tunaendelea kuwatafuta, ambao imesemekana wamekimbia baada ya kufanya tukio hilo,"amesema Kamanda Magomi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com