Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye leo tarehe 25 Aprili 2023 amekua Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 66 ya Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana iliyoko Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora.
Akizungumza katika Mahafali hayo, Mgeni Rasmi amewahimiza wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo ya Sekondari Tabora Wavulana kuona fahari ya kuchangia rasilimali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule kwa faida ya watoto wa kitanzania. ‘Nitumie fursa hii kuhimiza wanafunzi wote waliowahi kusoma katika shule hii kuona fahari kurejesha fadhila ’’ amesema Mkurugenzi Mkuu wa TEA.
Amepongeza uongozi wa shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana kwa kuzindua kanzidata ya wahitimu waliopitia shule hii yaani Alumni Database katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika mwezi Machi, 2023 na kusema hiyo ni hatua muhimu itakayowezesha kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili shule.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tabora Wavulana Bw. Deograsias Ali Mwambuzi ameishukuru Mamlaka ya Elimu kwa kufanya ukarabati mkubwa katika shule hiyo hatua ambayo amesema imechangia wanafunzi hao kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa. ‘Tunayo heshima kubwa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kushughulikia changamoto za elimu’ ameongeza Mwambuzi.
Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana ni miongoni mwa shule kongwe 17 ambazo Mamlaka ya Elimu Tanzania kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ilitoa ufadhili kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa madarasa, jengo la utawala, bweni kubwa la kihistoria na miundombinu ya maji safi na maji taka. Aidha ufadhili huo ulihusisha ujenzi wa maktaba na matenki ya maji.
Jumla ya wanafunzi 109 wanahitimu mafunzo ya kidato cha sita katika mwaka 2023 katika tahasusi za PCB, PCM na HGL.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye (kulia) akitoa cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana iliyoko Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye (kati kati) akiwa na wenyeji wake Mwenyekiti wa Bodi Bw. Paskali Kilagula (kulia) na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana Bw. Deograsias Ali Mwambuzi (kushoto) alipowasili shuleni hapo.Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Idete waliohudhuria Mahafali ya 66 ya Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana iliyoko Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora wakizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye (kushoto).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye (kulia) akitoa cheti na zawadi kwa mwalimu Wilifrida Selastine Shao kutokana na kuwezesha ufaulu mkubwa wa somo la Kemia katika Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana iliyoko Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora.
Social Plugin