Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN TARURA MKOA WA RUVUMA KAZI INAENDELEA

KATIKA kipindi cha miaka mwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa Mkoa wa Ruvuma zimeimarika maradufu.

Hatua hii imetokana na uamuzi wa dhati wa Rais Samia wa kuongeza bajeti kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Ruvuka kwa zaidi ya mara mara tatu.

TARURA Mkoa wa Ruvuma inahudumia jumla ya kilomita 7,146.202 za barabara, kati ya hizo kilomita 2,312.83 sawa na asilimia 32.36 ni za mjazio, kilomita 3,873.85 sawa na asilimia 52,85 ni mkusanyo na kilomita 959.52 sawa na asilimia 13.43 ya mtandao mzima wa mkoa ni za jamii/kijiji.

Anapozungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Samia, Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Wahabu Nyamzungu anasema mwaka 2020/21 mkoa ulitengewa Sh bilioni 7.973 za Mfuko wa barabara zilizotumika kufanya matengenezo ya kawaida ya kilomita 549.61 kwa Sh bilioni 1.356, sehemu korofi kilomita 137.29 kwa Sh bilioni 1.165, madaraja madogo 4, boksi kalavati 17, makalavati 11, madrifti 5 na mifereji ya maji yenye urefu wa mita 2,000 kwa gharama ya Sh bilioni 1.113,

Anasema hali ya mtandao wa barabara ulikuwa na kilomita 890.449 za barabara za changarawe sawa na asilimia 12.46, kilomita 93.635 barabara za lami sawa na asilimia 1.31, kilomita 3.92 barabara za zege na kilomita 6,159.19 zilikuwa barabara za udongo ambazo ni asilimia 12.46.

Anasema kuwa barabara zenye hali nzuri zilikuwa ni kilomita 1,391.453, hali ya kuridhisha kilomita 1,572.083, hali isiyoridhisha kilomita 4,182.667, madaraja 471, makaravati 1,940 na drifti 63.
“ Kwa kweli hali ya utekelezaji wa miradi ya barabara ilikuwa changamoto kubwa kwa kuwa bajeti ya utekelezaji wa miradi kwa mwaka ilikuwa finyu.”

Mhandisi Nyamzungu anasema kuwa mwaka 2021/22 ikiwa ni ndani ya miaka mwili ya uongozi wa Rais Samia TARURA Mkoa wa Ruvuma ulitengewa Sh bilioni 20.166 ambazo za tozo ya mafuta ni Sh bilioni 7, fedha za jimbo Sh bilioni 4.5, mfuko wa barabara Sh bilioni 7.383 na mfuko wa maendeleo Sh bilioni 1.283.

Anasema kwa mwaka 2022/23 Mkoa wa Ruvuma imetengewa bajeti ya Sh bilioni 23.757 na kati ya hizo fedha za tozo ya mafuta ni Sh bilioni 10.025, mfuko wa barabara ni Sh bilioni 6.918, fedha za miradi ya maendeleo ni Sh bilioni 1.39 na fedha za majimbo Sh bilioni 4.5.

“ Hivyo kwa miaka mwili ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan TARURA Mkoa wa Ruvuma tumepokea shilingi bilioni 43.924 zikiwa ni fedha za matengenezo ya barabara na madaraja.”
Anasema baada ya ongezeko la bajeti hali ya barabara kwa Mkoa wa Ruvuma imeimarika zaidi ambapo kilomita 1,372.581 ni barabara za changarawe, kilomita 118.688 ni barabara za lami, kilomita 6.92 ni barabara za zege na kilomita 5,658.41 ni barabara za udongo.

“Kwa sasa barabara zinazopitika kwa mwaka mzima zimefikia asilimia 35. Pia barabara zenye hali nzuri ni kilomita 2.250.387, zenye hali ya kuridhisha ni kilomita 1,767.889 na zile zilizo katika hali isiyoridhisha ni kilomita 3,127.913 na kuna madaraja 511, makalavati 2,130 na drifti 63.”

Anasema pia utekelezaji wa miradi ya barabara kwa sasa imeimarika ambapo ndani ya miaka mwili TARURA Mkoa wa Ruvuma umefanya matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 482.132, ujenzi wa barabara za lami kilomita 25.053, ujenzi wa madaraja 40, ujenzi wa mifereji ya maji ya mua urefu wa mita 3,400.

Pia ujenzi wa barabara za zege katika maeneo yenye miinuko na miteremko kilomita 6.92, ufunguzi wa barabara mpya kilomita 500.03 ambazo hazijawahi kufunguliwa tangu tupate uhuru na kupunguza kiwango cha barabara za udongo kutoka kilomita 6,159.19 hadi kufikia kilomita 5,658.41.
Aidha, ongezeko la uwekaji wa taa za barabarani imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka idai ya taa 34- hadi kufikia taa 383 ikiwa bado idadi ya taa zinazotarajiwa kuweka mpaka kufikia Juni mwaka huu kufikia taa 420.

Mhandisi Nyamzungu anataja baadhi ya miradi ya kimkakati ambayo TARURA Mkoa wa Ruvuma imeitekeleza katika kipindi hicho ni ujenzi wa barabara ya Luhindo-Mpepo-darpori kwa kiwango cha changarawe urefu wa kilomita 27.52.

“Barabara hii imeongeza tija kwa wakulima wa kahawa na sekta ya usafiri na usafirishaji kwani kabla ya maboresho gari zilizokuwa zikitumiwa na wananchi wa Kata ya Mpepo ni landrover pekee lakini sasa basi za abiria zimeweza kufika.”

Mhandisi Nyamzungu anasema pia kufungua barabara za fukwe za Ziwa Nyasa kwa ajili ya kuhamasisha utalii katika Wilaya ya Nyasa ambazo zimeboreshwa kwa fedha za tozo za mafuta.

“Eneo la fukwe za Nyasa kata ya Kilosa na Mbamba Bay halikuwa na barabara zilizoboreshwa lakini katika kipindi cha miaka mwili ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tumeweza kufungua kilomita 14 za barabara za changarawe, barabara hizi zitaboresha na kuleta hamasa katika sekta ya utalii wa picha na kufutia wawekezaji wa ufukweni.”

Mhandisi Nyamzungu anasema pia kuondoa vikwazo kwa kujengwa madaraja na makalavati, kujenga barabara za lami kwenye katika miji na makao makuu ya kila wilaya, kufungua barabara mpya hasa katika maeneo ya uwekezaji mkubwa wa sekta ya kilimo na uchimbaji wa makaa ya mawe.

Kuendeleza barabara za mitaa kwa kiwango cha changarawe na kuweka taa katika miji mbalimbali kwenye maeneo ya miji.

“Tunachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuongoza kwa mafanikio hasa katika sekta ya mundombini na kuondoa vikwazo vya usafiri na usafirishaji wa mazao vijijini.”

“ Kwa kuongeza fedha kumeongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa miradi, kuinua uchumi kwa wananachi wa kawaida hasa wakulima kwa kuwawezesha kusafirisha mazao ya kwa urahisi kuyafikia masoko na hatimaye kukidhi mahitaji yao kwa urahisi.”

Mhandisi Nyamzungu anaongeza: “tunamwomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kutuwezesha TARURA ili tuweze kutimia kauli mbiu yetu isemayo ‘Tunakufungulia barabara kufika kusikofikika’.”




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com