TBS KANDA YA KATI YATEKETEZA BIDHAA ZISIZOFAA KWA BINADAMU YATOA MAAGIZO MATANO KWA WAFANYABIASHARA

 
Bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vipodozi zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata vyenye sumu vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 33 vikiteketezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya kati,leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma.

 
Afisa Mthibiti Ubora wa TBS Kanda ya Kati Bw.Sileja Lushibika ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuteketeza Bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vipodozi zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata vyenye sumu vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 33 leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma.
Afisa Usalama wa Chakula TBS Kanda ya Kati Bi.Sifa Chamgenzi ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuteketeza Bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vipodozi zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata vyenye sumu vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 33 leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma.

Alex Sonna-DODOMA

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya kati, limeteketeza bidhaa za vyakula na vipodozi zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata vyenye sumu vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 33 huku ikitoa maagizo matano kwa wafanyabiashara.

Hayo yameelezwa leo,Aprili 6,2023 jijini Dodoma na Afisa Mthibiti Ubora wa TBS Kanda ya Kati Bw.Sileja Lushibika wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.

Bw.Lushibika amesema jumla ya kilo 3509.09 zenye thamani ya zaidi Sh milioni 33 zimeteketezwa,ikijumuisha bidhaa za chakula ambazo ni kilo 2098.727 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 21 na vipodozi kilo 1410.303 vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 21.

Amesema bidhaa zikizoteketezwa zimetokana na kaguzi zilizofanyika katika maeneo ya biashara,baa,hoteli na stoo zilizopo katika Halmashauri zote za Mikoa ya Dodoma,Singida na Tabora katika kipindi cha Agosti 2022 hadi Machi 2023.

"Uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zile zenye viambato sumu zinaathiri uchumi wa Nchi pamoja na afya za Watumishi,"amesema Bw.Lushibika

Amesema bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na zile ambazo tarehe ya mwisho wa matumizi zimehaririwa zinaathiri upatikanaji wa virutubisho vinavyotegemewa zinaweza kusababisha magonjwa ya muda mfupi na mrefu ikiwemo saratani.

Ofisa huyo amesema kwa upande wa vipodozi vile vyenye viambata vyenye sumu athari zake ni za muda mfupi na mrefu ikiwemo kuathiri ngozi,macho,mfumo wa uzazi kwa kina mama,ukuaji kwa watoto na magonjwa ya saratani hasa ngozi.

Lushibika ametoa wito kwa wafanyabiashara kukagua bidhaa zao mara kwa mara ili kujiridhisha ubora wake,kutunza bidhaa hizo kwa mujibu wa taratibu za wazalishaji.

Pia,kuepuka kuuza bidhaa za vipodozi zenye viambato sumu,kuacha mara moja kuhariri taarifa za mwisho wa matumizi na wazalishaji wa bidhaa kuthibitisha bidhaa zao.

"Wananchi wanaomba kutoa ushirikiano,kwa Shirika la Viwango TBS endapo watakutana na bidhaa ambazo wanazitilia Mashaka,"amesema Bw.Lushibika

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post