Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YATOA LESENI NA VYETI 29 KWA WAJASIRIAMALI

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limekabidhi vyeti na leseni za kutumia alama ya ubora kwa wazalishaji 29 wa bidhaa zilizokidhi viwango kutoka Kanda ya Kati kwenye mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na wazalishaji wa kanda ya nyanda za juu kusini kwa mkoa wa Iringa.

Kati ya hizo leseni na vyeti vipatavyo 20 vimetolewa kwa wajasiriamali wadogo na waliobaki tisa (9) ni wazalishaji wakubwa.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa leseni vyeti hivyo leo Aprili 28,2023 Jijini Dodoma, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Mhe.Ally Gugu amesema ni wajibu wetu sote kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa viwandani, zinazingatia kanuni bora za uzalishaji ambazo hazitachafua wala kuharibu sifa halisi za bidhaa husika.

"Kwa kulitekeleza hili Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa kisekta (kama ninyi hivi leo) kwa lengo la kulinda afya za watumiaji na mazingira katika Mkoa wetu wa Dodoma, Kanda ya Kati na maeneo mengine nchini". Amesema

Amesema bidhaa ikithibitishwa bora wake na nchi wanachama ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki, bidhaa hiyo itaingia katika nchi wanachama pasipo kukaguliwa na kupimwa tena ili kutambua bora wake.

Aidha amewaasa wazalishaji wa bidhaa ambao wamekabidhiwa leseni na vyeti kuendelea kuzalisha bidhaa kwa kufuata viwango na maelekezo watakayopewa na wataalam kutoka Shirika la Viwango Tanzania.

Amesema Serikali kupitia TBS ithakikisha miongozo na taarifa muhimu kuhusiana na ubora na usalama wa bidhaa zinapatikana kwa wakati na kuhakikisha bidhaa zenye ubora hafifu zinaondolewa sokoni lakini pia kuendelea kutoa elimu elekezi wakati wa kaguzi mbalimbali viwandani na masokoni.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kati Bw.Nickonia mwambene akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TBS ameipongeza Serikali i kwa kuendelea kulipia gharama za kuwahudumia wajasiriamali wadogo katika ukaguzi na upimaji wa bidhaa zao.

"Jumla ya Shilingi Milioni 250 zinatengwa kila mwaka kuwahudumia Wajasiriamali wadogo bure kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya mwanzo, ambapo baada ya hapo hutakiwa kuanza kuchangia 25% hadi 100% mwaka wa 7". Amesema

Amesema ugawaji wa leseni na vyeti hivyo utasaidia kuongeza imani kwa umma juu ya ubora wa bidhaa na kuweza kukubalika sokoni na pia italeta faida ya kiushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com