Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua kampeni ya kuongeza uelewa kwa umma kuhusu huduma za posta na usafirishaji wa mizigo kwa leseni na umuhimu wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, amesema kampeni hiyo inalenga kukabiliana na changamoto zinazokabili watumiaji wa huduma za usafirishaji wa vipeto na vifurushi.
Alifafanua kuwa leseni kwa watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto zinaongeza uwajibikaji wa watoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.
Kampeni hiyo ya elimu kwa umma inalenga kuwahamasisha wananchi kutumia watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi walioidhinishwa na kusajiliwa rasmi, ambazo zina ofisi zilizo rasmi, stoo za kuhifadhia vipeto na vifurushi na rekodi nzuri ya ufanisi, usalama, na uadilifu katika utoaji huduma za kusafirisha vipeto na vifurushi.
“Usafirishaji wa vipeto na vifurushi unatembeza shughuli zetu za uchumi, sisi kama mamlaka, sekta ya Posta ni sehemu ya eneo letu la usimamizi, hivyo tunao wajibu wa kuwakumbusha watoa huduma waliopo na wanaotoa huduma za kiposta au zinazohusiana na huduma za posta kama usafirishaji vifurushi na vipeto kuhakikisha wanasajili huduma zao hapa TCRA na wale ambao leseni zao zimefikia ukomo wahuishe leseni hizo.
Mkurugenzi Mkuu Bakari aliwakumbusha watoa huduma za usafirishaji vifurushi na vipeto yakiwemo mabasi ya abiria kwamba kufanya kazi za usafirishaji vifurushi na vipeto bila leseni ni kutenda kinyume na utaratibu wa sheria.
TCRA ilielekeza kwamba wanaohitaji kusajili shughuli hizo wanaweza kutuma maombi ya kusajiliwa kupitia lango la watoa huduma za Mawasiliano la TCRA linalopatikana mtandaoni kupitia ukurasa wa Tanzanite Portal unaomwezesha mwombaji kutolazimika kufika Ofisi za TCRA.
“Tumeboresha sana huduma zetu waombaji leseni zote za mawasiliano wanaweza kupata leseni hizo kwa njia ya lango la Tanzanite,” alisisitiza.
TCRA inatoa leseni kwa kampuni za posta na usafirishaji wa mizigo katika makundi sita, ikiwa ni pamoja na kimataifa, Afrika Mashariki, ndani ya jiji, na katikati ya majiji.
Katika kampeni ya miezi minne kuanzia mwezi Machi, watumiaji huduma za usafirishaji vipeto na vifurushi watapewa elimu kuhusu hatari za kutumia huduma za watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto wasio na leseni ya TCRA; pia, watapewa Elimu kuhusu haki zao kama watumiaji kuhakikisha zinazingatiwa.
Haki za watumiaji wa huduma za kiposta ni pamoja na kupata taarifa kabla na baada ya huduma kushughulikiwa kwa malalamiko na kupata nafasi ya kukata rufani kwa Mdhibiti, miongoni mwa mengine.
Takwimu za hivi karibuni zilizochapishwa na TCRA zinaonyesha ongezeko la usafirishaji wa vifurushi na vipeto nchini Tanzania kutokana na ukuaji wa biashara mtandaoni. TCRA ilisisitiza watumiaji kuhakikisha wanajiridhisha na uhalali wa huduma za watoa huduma wanaowachagua kuwapatia huduma.
Social Plugin