UZINDUZI WA MKUTANO WA 31 WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


Serikali inafanya mageuzi katika sekta ya elimu kwa kuwa na sera na mitaala itakayowezesha wahitimu kuwa na Maarifa, Stadi, ujuzi utakaowawezesha kujiamini, kujiajiri na kuajirika katika mazingira ya utandawazi na kukidhi mahitaji ya soko.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo wakati akimuakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika uzinduzi wa Mkutano wa 31 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara uliofanyika jijini Arusha.

Katibu Mkuu huyo amesema wizara inaendelea kutekeleza vipaumbele vilivyoinishwa katika bajeti ya mwaka 2022/23 ambavyo ni mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Sheria mbalimbali, mabadiliko ya Mitaala pamoja na kuangalia suala zima la idadi na ubora stahiki wa walimu, wakufunzi na wahadhiri pamoja na mahitaji ya miundombinu na vitendea kazi.

“Nitoe rai kwa Menejimenti, Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara na Watumishi wote kwa ujumla kwa pamoja tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha kuwa tunafanya kazi kwa bidii, weledi na nidhamu ya hali ya juu katika kutekeleza majukumu ya wizara yetu kwa ufanisi ili elimu inayotolewa nchini iwe katika kiwango bora na cha ushindani kitaifa na kimataifa” amesema Katibu Mkuu huyo

Prof. Nombo ameongeza kuwa wizara imeshafanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na imekamilisha Rasimu ya Sera toleo la Mwaka 2023, ambapo kwa sasa inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau ili kukamilisha mchakato wa uandishi wa Sera Elimu na Mafunzo itakayozingatia mahitaji ya jamii na soko la ajira la ndani na nje pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Aidha, amewataka watumishi wa wizara hiyo kutumia mafunzo mbalimbali wanayopata kufanya kazi kwa umahiri katika kusimamia na kushiriki ipasavyo katika hatua zote za utekelezaji wa Sera na Mitalaa inayohuishwa ili kuleta tija katika kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia jambo ambalo litawezesha vijana kuwa na uwezo, ujuzi, maarifa, umahiri na ubunifu stahiki na kuweza kuingia katika ushindani wa soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongela ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika katika mabadiliko ya mitaala na mapitio ya Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo yanalenga kuwajengea vijana wa kitanzania umahiri na ujasiri utakao wawezesha kushindana katika soko la Dunia la ajira.

Mhe. Mtahengerwa amewaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa Serikali inatambua uwepo na mchango wa mabaraza ya wafanya kazi nakuwataka kuwa watetezi wa watu na kuacha kutumika kisiasa, huku akisisitiza umuhimu wakutumia lugha za staha wakati wa kuwasilisha hoja na mambo muhimu yanayolenga kuinua hali za wafanya kazi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula amesema baraza la wafanyakazi ni matokeo ya sera ya kuwashirikisha wafanyakazi mambo mbalimbali yanayotokea kwenye maeneo ya kazi, hivyo uwepo wa mkutano huu ni utekelezaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya ushirikishwaji na majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma.

Naye Katibu wa Baraza hilo Huruma Mageni amesema kauli Mbiu ya Mwaka 2023 ya Baraza hilo ni “Sera na Mitaala Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, kauli ambayo inasadifu umuhimu wa kuwa na mitaala pamoja na Sera zinazoendana na mahitaji ya sasa ya sayansi na teknolojia ili kuwafanya vijana wa kitanzania kuajirika na kujiajiri

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post