Na Dotto Kwilasa , Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limewathibiti majambazi wanne wa kiume ambao majina yao bado hayajatambulika wenye umri kati ya 25-30 waliokuwa katika harakati za kufanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha nyumbani kwa Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la polisi Dodoma Martine Otieno tukio hilo limetokea Aprili 25,2023 majira ya saa 03:10 usiku mtaa wa Mwangaza, Kisasa Kata ya Dodoma Makulu.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 26,2023 Kamanda Otieno amesema majambazi hao walivamia nyumbani kwa Bi. Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara, mkazi wa Kisasa wakiwa wamevaa barakoa usoni na kufanikiwa kunyang'anya pesa taslim 1,100,000/= simu ya Samsung moja na simu ndogo tatu baada ya watu hao kumtishia kumkata mapanga ndipo mhanga alipiga kelele za kuomba msaada.
“Baada ya mhanga kupiga kelele za kuomba msaada zilisikika kwa majirani ambapo majirani hao walitoa taarifa kwa askari waliokuwa doria eneo hilo ambao walifika kwa haraka na kuwakuta watu hao ambao walijihami kwa kutaka kuwashambulia askari kwa mapanga na askari hao kujibu mapigo kwa kuwafyatulia risasi ambazo ziliwajeruhi watuhumiwa hao maeneo mbalimbali ya miili yao,”amesema.
Ameongeza kuwa majambazi hao walijificha nyuma ya ukuta wa fensi na kuruka ukuta huo na kwenda kumvizia Edna Joseph Kashashari wakati anataka kufunga mlango wa nyumba na kumtishia kumkata na mapanga kisha kumpora vitu hivyo.
Hata hivyo amesema watu hao wamefariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
“Wamepata walichostahili,hiyo ndiyo adhabu yao,Kwa yeyote ambaye hajamuona ndugu yake anaweza kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuona miili hiyo kubaini kama ni ndugu yake,"amesisitiza
Social Plugin