Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa ufafanuzi wa viwanja vinavyomilikiwa kampuni ya Slipway Towers Ltd vilivyopo Msasani Peninsula jijini Dar es Salaam ambapo amemuagiza katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng. Anthony Sanga kuchunguza kubaini kama kuna wataalam waliohusika katika upotoshaji huo ili waweze kuchukuliwa hatua za haraka za kinidhamu.
Aidha, Dkt Mabula ameelekeza kuwa, kuanzia sasa Manispaa ya Kinondoni inapotaka kupangisha maeneo au eneo ambalo ni kwa matumizi ya umma inatakiwa kijiridhisha kwanza kwa lengo la kujua eneo husika kama mipaka yake haijaingiliana na wapangishaji wengine ili kuepuka migogoro.
Kumbukumbu za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinaonesha kuwa viwanja namba 1497, 1498 na 1856 vinamilikiwa kampuni ya Slipway Towers Limited kwa hati namba 29035 ya muda wa miaka 99 iliyotolewa Januari 1, 1980 kwa ukubwa wa hekta 1.383 kama ilivyo kwenye ramani ya usajili namba 18460 ya mwaka 1980.
Hata hivyo, upimaji wa viwanja ulirejewa na kufanyiwa maboresho yaliyoongeza kiwanja namna 1967 ambapo kampuni ya Slipway Towers Ltd iliomba kiwanja husika kuunganishwa kwenye hati moja na maombi kukubaliwa na kusajiliwa Agosti 13, 1998 ambapo ukubwa uliongezeka kutoka hekta 1.383 hadi 1.8759.
Waziri Mabula alitoa ufafanuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 29 April 2023 kufuatia malalamiko yaliyotolewa na mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Somgoro Mnyonge kuhusu umiliki na uendelezaji wa eneo katika viwanja hivyo.
"Ieleweke wazi kuwa mhe. Dkt Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akivutia wawekezaji wengi nchini katika sekta mbalimbali kwa maslahi mapana ya nchi yetu hivyo serikali haitavumilia vitendo vinavyoenda kinyume na azma ya rais kuvutia wawekezaji na tanzania ni sehemu salama kuwekeza" alisema Dkt Mabula.
Amemuelekeza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala kusimamia taratibu zote katika kipindi cha mpito wakati mgogoro katika eneo hilo ukishughulikiwa sambamba na kusimamia pale inapotokea changamoto yoyote kwa kuangalia namna bora ya kufanya mawasiliano kabla ya kutolewa matamko yenye kuleta upinzani.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, uhakiki uliofanywa na wataalam wa wizara yake umebaini kuwa, siyo kweli kwamba mwekezaji kampuni ya Slipway Towers Limited imeingia baharini kwa mita 850 bali zilizotajwa ni mita za mraba ambazo Manispaa ya Kinondoni imempangisha kampuni ya Dorishers ndani ya kiwanja cha hati milki namba 29035 kinachomilikiwa na kampuni ya Slipway Towers Limited.
"Tangu mwaka 1998 hadi sasa wizara haijapata maombi ya Slipway kufanya mabadiliko yoyote kwenye ramani au hati miki na hakuna jambo lolote wizarani linalohusiana na upimaji au umilikishaji unaohusina na kampuni ya Slipway towers ltd, kilichosemwa na meya wa manispaa ya kinondoni kuwa kuna mchakato unaoendelea ndani ya wizara hakipo na hakuna mchakato wala maombi". Alisema Waziri Mabula.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mpango wa uendelezaji upya eneo la Masaki yaani Masaki-Oyesterbay Development Plan ya 2011-2031 ulijadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziti hivyo marekebisho yoyote ya mpango wa eneo hilo lazima yapitishwe na Baraza la Mawaziri.
"Kwa hiyo wizara kama wizara hakuna inachoweza kufanya mabadiliko hayo kwa sababu tayari yapo katika mpango wa uendellezaji ulioasisiwa na Baraza la Mawaziri na marekebisho yoyote lazima yapitishwe na baraza hilo". Alifafanua Dkt Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akifafanua jambo wakati wa kikao chake na waandishi wa habari kufafanua upotoshaji wa viwanja vinavyomilikiwa na kampuni ya Slipway Towers Ltd tarehe 29 April 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Slaam wakati wa kutoa ufafanua wa upotoshaji wa viwanja vinavyomilikiwa na kampuni ya Slipway Towers Ltd tarehe 29 April 2023.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Eng. Anthony Sanga (Kulia) pamoja na Mpima wa Wizara ya Ardhi Romanus Sanga wakati wa kikao cha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 29 April 2023. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Social Plugin