Na Mwandishi wetu- Tabora
Zaidi ya wagonjwa 410 wamepata matibabu ya kibingwa na kibobezi katika kambi maalum ya siku 5 iliyofanyika katika hospitali ya Rufaa Nkinga, Tabora kwa ushirikiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na hospitali ya Rufaa Nkinga ambapo wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji mkubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Rufaa Nkinga Mr. Victor Ntundwe amewashukuru Madaktari bingwa, Wauguzi na Mtaalam wa usingizi wa Taasisi ya MOI kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kambi hiyo ambayo imewajengea uwezo wataalam wa hospitali ya Rufaa Nkinga
“Tumepata shuhuda nyingi kutoka kwa wagonjwa mbalimbali ambao walikuwa hawana uwezo wa kwenda Dar es Salaam kuzifuata huduma hizo na wamefurahi sana kuona huduma hizo zinatolewa hapa hospitali ya Rufaa Nkinga ” Alisema Bw. Ntundwe
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema wamefanya kambi hiyo kwa lengo la kujengeana uwezo wa kutoa tiba bobezi ambazo zinapatikana katika hospitali ya MOI.
“Tunatekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi karibu na wananchi na kambi hii itakuwa endelevu kila baada ya muda Fulani wataalam wa MOI watakuwa wanakuja hapa” amesema Dkt. Boniface
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali ya Rufaa Nkinga Dkt. Tito Chaula amesema kulikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za tiba bobezi ukanda wa magharibi na zaidi ya wagonjwa 410 wametibiwa katika kambi hiyo na wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.
Afisa Muuguzi kutoka kitengo cha upasuaji MOI Bi. Jane Mdalingwa amesema kwa muda waliokuwa pamoja wameweza kufundishana viwango ya chumba cha upasuaji inavyotakiwa ili mgonjwa anavyofanyiwa upasuaji asipate maambukizi yeyote na maandalizi ya mgonjwa kabla hajaingia chumba cha upasuaji.
Mkazi wa Geita Edina Joramu ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kusogeza tiba za kibobezi mkoani Tabora kwani angetumia gharama Zaidi kwa kufuata huduma hizo Mwanza, Dodoma au Dar es Salaam.
Social Plugin