Mahakama nchini Kenya imeagiza kuzuiliwa kwa akaunti 15 za benki zinazomilikiwa na mchungaji mwenye utata Ezekiel Odero kwa siku 30.
Hii inafuatia ombi lililowasilishwa na Ofisi ya Mkurungenzi mkuu wa upelelesji wa Mashitaka (DCI) kutaka akaunti zote zizuiliwe wakati uchunguzi ukiendelea.
Katika waraka uliowasilishwa mahakamani, DCI, ilidai Mchungaji Ezekiel wa Kanisa la New Life Prayer Centre anashukiwa kwa utakatishaji wa pesa kutokana na uhusiano na Mchungaji Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International , ambaye anachunguzwa kwa madai ya kuwalaghai wafuasi wa kanisa lake kufunga hadi kufa ili ‘’kukutana na Yesu’’.
Wapelelezi waliiambia mahakama kuwa akaunti za benki za Mchungazji zimekuwa zikipokea kiasi kikubwa sana cha pesa ambazo pesa zake zinashukiwa kuwa haramuzilizotoka kwa wahanga ambao wanadaiwa kulaghaiwa kuuza mali zao na kumpatia mchungani Mackenzie.
Wameitaka mahakama kuwaruhusu kuzifikia akaunti kadhaa za benki katika Equity Bank, Co-op Bank, KCB na HFC Bank.
Kulingana na afisa wa polisi anayefanyia uchunguzi DCI, Martin Munene DCI, wanahofu kuwa pesa zilizoshikiliwa katika akaunti mbali mbali za benki zitahamishwa iwapo mahakama haitatoa agizo la kuzifikia akaunti hizo.
Wiki iliyopita mchungaji Ezekiel alikwenda katika Mahakama ya juu zaidi mjini Mombasa akitaka kuzuia kufujwa kwa akaunti zake.
Mchungaji Ezekiel alikuwa amedai kuwa kushikiliwa kwa akaunti zake kutakuwa ni kuingilia uhuru wake na wa kanisa waumini wa kanisa lake.
Suala hilo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Jumanne mahakamani.
Chanzo - BBC SWAHILI