Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wapili kushoto), Kahumbya Bashige, Mjumbe wa Bodi ya CRDB Bank Burundi (wapili kulia), Katibu wa Kampuni Benki ya CRDB, John Rugambo (wakwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (wakawanza kulia) wakionyesha Taarifa ya Mwaka 2022 ya Benki ya CRDB wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuwakaribisha wanahisa wa benki hiyo katika Mkutano Mkuu wa 28 utakaofanyika siku ya jumamosi ya tarehe 20 Mei 2023. Picha zote na Othman Michuzi.
======= ====== ========
Arusha 16 Mei 2022 - Benki ya CRDB inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa siku ya Jumamosi tarehe Mei 20 kuanzia saa 2 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Mkutano huo unafanyika kufuatana na Sheria ya Makampuni namba 212 ya mwaka 2002, ambapo kila mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo unaowapa Wanahisa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha au kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki.
Akizungumzia katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay amesema mkutano huo utafanyika kwa njia mseto “Hybrid Meeting” ili kutoa fursa kwa wanahisa wengi zaidi kushiriki kwa njia ya kidijitali.
Dkt. Laay alisema katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa waliadhimia Mkutano wa 28 wa ufanyike Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, lakini kwa kuzingatia mkakati mpya wa Benki wa 2023-2027, Bodi ya Wakurugenzi ilipitia na kuidhinisha mabadiliko ya eneo la Mkutano kwenda Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
“Bodi ya Wakurugenzi ilipendekeza mabadiliko hayo ya sehemu ya kufanyika Mkutano Mkuu kwa Wanahisa wanaomiliki zaidi ya 50% kulingana na Katiba na Mkataba wa Benki (MEMARTS) na Sheria ya Makampuni Na. 12 ya 2002, na Wanahisa walikubali mabadiliko haya,” alisema Dkt. Laay huku akiwakaribisha wanahisa katika Mkutano huo.
Dkt. Laay alisema Mkutano huo pia utafanyika kupitia mtandaoni Wanahisa wataweza kujiunga kuanzia saa 2:00 asubuhi kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App, ambapo imewekwa sehemu ya ya kujisajili kushiriki Mkutano Mkuu.
“Tumeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa,” alisema Dkt. Laay huku akiwahakikishia kuwa Benki hiyo vizuri katika kuhakikisha wanashiriki bila chanagamoto yoyote.
Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utatanguliwa na semina maalum kwa wanahisa na umma yenye kauli mbiu ya “Ushirika wa Serikali na Benki ya CRDB kuwezesha Vijana na Wanawake kupitia programu ya IMBEJU”. Semina hiyo ambayo pia itaambatana na maonyesho ya vijana wabunifu itafanyika siku ya Ijumaa tarehe 21/05/2022 kuanzia saa 3 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Mgeni Rasmi katika semina hiyo anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mh. Mwigulu Nchemba ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wa masuala ya fedha, sheria na uwekezaji katika masoko ya mitaji.
Ajenda mbalimbali zitajadiliwa katika Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ni pamoja na uchaguzi wa wajumbe huru wa bodi, kuteua wakaguzi wa hesabu, na kujadili na kupokea Taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi, na Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa, pamoja na gawio kwa mwaka 2022 ambapo pendekezo la gawio la Sh 45 kwa hisa litawasilishwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, alisema pendekeo hilo la ongezeko la gawio kwa hisa linatokana na Benki ya CRDB kuendelea kupata matokeo mazuri sokoni ambapo mwaka wa fedha ulioisha ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi 351.4 bilioni ukilinganisha na Shilingi 268 bilioni mwaka 2021.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema katika mkutano mkuu wa 28 wanahisa wa benki hiyo watapata nafasi ya kujadili juu ya mkakati mpya wa biashara wa muda wa kati wa miaka mitano 2023 – 2027.
Mkakati huu ambao umebebwa na kaulimbiu ya “Mageuzi Tahabiti” una lenga katika kuimarisha utendaji wa Benki ya CRDB na kuifanya kuwa kinara katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.
Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha wanahisa wa Benki ya CRDB kujitokeza kwa wingi kwani ushiriki wao utaiwezesha Bodi na Menejiment kupata maoni yao ya namna bora ya kuboresha utendaji wetu.
Akielezea kauli mbiu ya Mkutano wa mwaka huu wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ya “Mageuzi Thabiti” Mkurugenzi wa Mawasiliano wa benki hiyo, Tully Mwambapa alisema inaelezea namna inavyoimarika katika utendaji kutokana na mabadiliko ya kimkakati yanayofanywa kila mwaka na kuifanya iwe na ukuaji endelevu wenye thamani ya uwekezaji.