Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA ELIMU YAOMBA KUIDHINISHIWA ZAIDI YA SH.TRILIONI 1.678


WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda,akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024,leo Mei 16,2023 bungeni jijini Dodoma .

Na Alex Sonna-DODOMA

KATIKA mwaka wa fedha 2023/24, Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu, kuwezesha vijana wa kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika huku ikiliomba bunge kuidhinisha zaidi ya Sh.Trilioni 1.678.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Machi 16,2023 bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023-2024.

Waziri Mkenda amevitaja vipaumbele hivyo ni kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu na kuanza utekelezaji,kuongeza fursa na ubora wa mafunzo ya amali katika elimu ya sekondari na vyuo vya Kati vya Amali.

Pia, kuongeza fursa na ubora wa elimu ya msingi na sekondari,kuongeza fursa na ubora wa elimu ya juu; na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

ELIMU YA UFUNDI

Waziri Mkenda amesema serikali itaendelea kuhakikisha kuwa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi Stadi nchini inatolewa kwa vitendo kwa lengo la kukuza na kuendeleza ujuzi na umahiri.

“Itarasimisha ushirikiano na taasisi mashirikia 60 kutoka sekta rasmi kwa lengo la kuongeza fursa kwa wanafunzi na walimu wa elimu ya mafunzo ya ufundi stadi ili kuwezesha wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo katika maeneo ya kazi,”amesema Prof Mkenda.

Pia amesema Wizara itanunua vifaa vya kisasa vitakavyotumika katika maabara ya udongo, maji na mimea katika Chuo cha Ufundi Arusha ili kuongeza uzalishaji na utoaji wa ushauri wa kitaalamu.

Pia amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa inawezesha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia katika vyuo vya ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi.

Vilevile, itaendelea kuwakutanisha wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kubadilishana uzoefu na kupendekeza namna bora ya kuendeleza ubunifu unaopatikana nchini.

VYUO 64

Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi 64 katika wilaya ambazo hazina vyuo hivyo pamoja na ujenzi wa Chuo cha Mkoa wa Songwe na itaanza kutoa mafunzo ya amali katika vyuo 29 vilivyokamilika.

Vilevile, itakamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya Chuo cha Ufundi Dodoma ambapo kukamilika kwa awamu hiyo kutawezesha kudahili wanafunzi 1,500.

UBORA WA ELIMU

Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea kuongeza fursa za Elimu kwa kutoa ithibati kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.

Amesema itasajili shule za msingi na sekondari takribani 560 ambapo awali pekee 20, awali na msingi 380 (Serikali 250 na zisizo za Serikali 130), sekondari 165 (Serikali 135 na zisizo za Serikali 30), chuo cha ualimu kimoja cha binafsi na nyingine kwa kuzingatia maombi yatakayowasilishwa na kukidhi vigezo.

“Itaanza kusajili shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wadau wengi zaidi,”amesema Prof Mkenda.

Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kutoa fursa za elimu na mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kutoa ushauri pamoja na utoaji wa mafunzo kazini.

UALIMU

Waziri Mkenda amesema katika kuimarisha elimu ya ualimu, Serikali itaendelea kuimarisha maandalizi ya walimu tarajali katika vyuo vya Ualimu.

Amesema itatoa mafunzo kwa vitendo kwa wanachuo wa Vyuo vya Ualimu zaidi ya 17,000 kwa lengo la kuhakikisha walimu tarajali wanapata stadi stahiki za ufundishaji na ujifunzaji.

“Itanunua vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vifaa vya maabara na kemikali katika Vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali,”amesema Waziri Mkenda.

VITABU

Prof Mkenda amesema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwa lengo la kuimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi na hivyo kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na kujenga tabia ya kujisomea.

“itachapa na kusambaza vitabu vya kiada na kiongozi cha Mwalimu kwa Elimu ya Awali nakala 6 kwa shule zinazotumia Kiswahili na nakala 6 kwa shule zinazotumia Kiingereza.

“ Darasa la kwanza nakala 6 kwa shule zinazotumia Kiswahili na nakala 6 kwa shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia.

“ Darasa la III nakala 12 kwa shule zinazotumia Kiswahili na nakala 12 kwa shule zinazotumia Kiingereza,vitabu vya kiada nakala 31 na Kiongozi cha Mwalimu nakala 31 kwa Kidato cha 1, vitabu vya kiada nakala 29 na kiongozi cha mwalimu nakala 29 kwa kidato cha 5,”amesema Waziri Mkenda.

UTAFITI

Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea kufanya tafiti katika ngazi ya elimu msingi, Sekondari na vyuo vya ualimu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutekeleza.

Amesema itafanya utafiti katika maeneo matatu na itatoa ushauri elekezi katika maeneo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa lengo la kutatua changamoto zinazojitokeza katika eneo la uongozi na usimamizi wa elimu.

Pia itafanya utafiti katika maeneo mawili ya tathmini ya upimaji wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Vilevile itafanya utafiti tatuzi katika maeneo matatu ya kielimu katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu kwa ajili ya kubaini mafanikio na changamoto za utoaji wa elimu nchini na kutoa mapendekezo stahiki.

TEHAMA

Amesema Serikali itaboresha mfumo wa kufundishia na kujifunzia kwa Elimu ya Sekondari na kuandaa maudhui ya kidijiti yatakayoimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia Tehama.

Pia itaendelea kuimarisha utoaji wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwa kutumia TEHAMA kupitia mfumo wa kujifunzia na kufundishia.

MIUNDOMBINU

Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya maktaba kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujisomea na kujifunza

“itaendelea na ujenzi wa jengo la maktaba ya Taifa Makao Makuu Dodoma litakalohifadhi nyaraka na machapisho kwa lengo la kutunza historia, maarifa, maadili, mila na desturi za Mtanzania.

“Itajenga maktaba ya Mkoa wa Singida ambayo itawezesha upatikanaji wa huduma za maktaba kwa wananchi zikiwemo huduma za rejea (reference sections), usomaji, kujifunza, utafiti na sehemu za huduma za jamii ikiwemo michezo ya watoto,”amesema Waziri Mkenda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com