GGML KILI CHALLENGE - 2023 KUKUSANYA BILIONI 2 KUDHIBITI VVU/UKIMWI

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa harambee ya uchangiaji wa fedha za kudhibiti maambukizi ya VVU/ Ukimwi kupitia kampeni hiyo ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2023. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu pamoja na wadau wengine waliohudhuria hafla hiyo.
Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa harambee ya uchangiaji wa fedha za kudhibiti maambukizi ya VVU/ Ukimwi kupitia kampeni hiyo ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2023.

NA MWANDISHI WETU
KAMPENI ya GGML Kili Challenge inayoratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) mwaka huu inatarajiwa kukusanya dola za Marekani milioni moja sawa na Shilingi za kitanzania bilioni 2.3.


Fedha hizo ambazo hukusanywa kila mwaka, hulenga kuchangia juhudi za serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu yaani kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.


Hayo yamebainishwa jana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo katika hafla ya uzinduzi wa harambee ya uchangiaji wa fedha hizo kupitia kampeni hiyo ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2023.


Mbali na kuishukuru Serikali kwa kuunga mkono kampeni hiyo iliyoasisiwa mwaka 2002, Shayo alisema wakiwa wadau wa mapambano haya ya UKIMWI na VVU, GGML imepokea msaada ambao uliiwezesha Kili Challenge kupiga hatua kubwa hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.


“Mwaka huu tumekuja tena kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo GGM kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) tunawakaribisha sana wadau wetu na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki kampeni hii.


“Kipekee tunapenda kutambua ushirikiano wa baadhi ya makampuni na taasisi mbalimbali ambazo tayari zimeshajitokeza kuchangia mfuko katika mwaka huu wa 2023. Nina imani wadau waliojitokeza leo watatusaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya kukusanya bilioni 2.3,” alisema.


Alisema VVU/UKIMWI bado ni tatizo kubwa nchini kwani takwimu za maambukizi mapya ya VVU haziridhishi, hususani kwa makundi maalum wakiwemo vijana.


Awali Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Hassan Babu aliipongeza GGML na TACAIDS kwa kuendelea kuutumia mlima Kilimanjaro kama kivutio kinachotumika kukusanya fedha kwa ajili ya mwitikio wa VVU na UKIMWI.
Alisema jambo hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika kuutangaza mlima huo maarufu duniani, na hivyo kuongeza idadi ya watalii.

“Nakaribisha mawazo, ushauri kutoka kwenu na wadau wengine wa jinsi ya kuboresha zaidi kampeni hii,” alisema.


“Natoa wito kwa watu binafsi, mashirika, taasisi na makampuni mengine kuiga mfano wa GGML kwa kujitoa zaidi kuchangia rasilimali za mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini, hususan katika kipindi hiki ambapo michango ya wahisani kutoka nje ya nchi inaendelea kupungua kwa sababu mbalimbali,” alisema.


Zoezi hilo la kupanda mlima linatarajiwa kuanza tarehe 14 Julai na kushuka tarehe 20 Julai mwaka huu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post