Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSANII WA NYIMBO ZA ASILI 'DAWA DAWA' ATUPWA JELA KWA KUMTUKANA RAIS SAMIA KWENYE WIMBO WAKE


Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

Msanii wa nyimbo za asili ya Kisukuma, Dawa Juma,mkazi wa kijiji cha Makurugusi wilayani Chato mkoani Geita,amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela au kulipa faini ya shilingi milioni 10 baada ya kupatikana na hatia ya kumtukana rais Samia Suluhu Hassan.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Chato,Amalia Mushi,baada ya mshitakiwa kukiri kosa mbele ya mahakama hiyo.

Awali Mwendesha Mashitaka wakili mwandamizi wa Serikali,Robert Magige,ameiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitunga wimbo wenye lengo la kumtukana matusi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,licha ya kujua wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Kwamba akiwa na nia ovu alirekodi wimbo huo na kuusambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kupeleka ujumbe wake kwa umma huku akijinadi kuwa haogopi kukamatwa.
Mwendesha mashitaka huyo,amesema kitendo cha kuchapisha taarifa za uongo na matusi kisha kusambaza kwenye mitandao ya kijamii (You tube) ni kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao,sheria namba 14 ya mwaka 2015.

Hata hivyo mshitakiwa baada ya kusomewa mashitaka yanayomkabili amekiri kutenda kosa hilo, licha ya kudai kuwa hakuwa na nia mbaya kwa kuwa alikusudia kuonyesha hali ilivyo mbaya kwa jamii baada ya bidhaa kupanda bei.

Aidha baada ya mshitakiwa kukiri kosa,wakili wa Serikali Magige ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye lengo la kumtukana rais kutokana na sababu zao binafsi.

Akitoa hukumu,hakimu wa mahakama hiyo,amesema kuwa kwa kuzingatia kuwa mshitakiwa hakuisumbua mahakama hiyo,kwa kukiri kosa kwa kinywa chake mwenyewe mahakama inamhukumu kifungo cha miaka sita jela au kulipa faini ya shilingi milioni 10.

Hata hivyo mshitakiwa amepelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo chake baada ya kushindwa kulipa faini iliyoelekezwa na mahakama hiyo.

CHANZO - JAMHURI MEDIA

Dawa dawa kali ni msanii wa nyimbo za asili lakini katika uimbaji wake amekuwa akimuimba mh. Samia Suluhu mara nyingi amekuwa akiimba huku akimkosoa Raisi kile anachokifanya na kuweka utani uliopitiliza kwenye nyimbo zake.

Huu hapa wimbo wa Msanii Ryamapetroli akimshauri msanii Dawa Dawa kuacha tabia ya kutukana

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com