Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Mhe.Bernard Kamilius Membe, amefariki dunia muda mfupi uliopita katika Hospitali ya Kairuki mkoani Dar es Salaam.
Taarifa kutoka ndani ya familia zinasema Membe amefariki dunia asubuhi ya leo Ijumaa, Mei 12; katika Hospitali ya Kairuki (HK) iliyoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam, akiwa anapatiwa matibabu, baada ya kupelekwa mapema leo kutokana na changamoto ya homa na kifua.
Membe ambaye anatajwa kama Kachero mbobevu, Mwanadiplomasia nguli na Mwanansiasa makini, aliwahi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2020, akipeperusha bendera ya ACT Wazalendo.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi. Pole kwa familia, ndugu, jamaa & marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina", Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Bernad Membe ni mmoja wa Wanadiplomasia, Jasusi na Mwanasiasa mahiri aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaitaifa, katika serikali ya awamu ya nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Social Plugin