Daktari wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje nchini Bernard Membe, ameondoa sintofahamu ya kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe na kusema hajauawa bali kifo chake kimetokana na maambukizi ya ghafla ya mapafu yaliyopelekea damu kuganda.
Daktari huyo binafsi wa Benard Membe, Profesa Harun Nyagori amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimechagizwa na ugonjwa wa maambukizi ya mfumo wa mapafu hewa.
Taarifa hiyo ya daktari inakuja kipindi ambacho kumekuwepo na taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu chanzo cha kifo chake.
Membe amefariki dunia leo, Ijumaa ya Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Hubert Kairuki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Profesa Harun amesema ugonjwa huo unasababisha mgando wa damu na kuzuia mapafu kupeleka hewa ya oksijeni.
"Hali hii inaweza kumkuta mtu yeyote mara tu anapopata maambukizi haya kwa njia ya hewa hata kwa wagonjwa wanaopata pneumonia pia inaweza kuwakuta.
"Kinachozungumzwa huko mtaani kwamba mzee ameuawa amepewa sumu sijui nini, hiyo iondoke, ukweli ni kwamba amefariki kwa maradhi ya kawaida," amesema Profesa Nyagori ambaye pia ni Mtaalamu wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Hata hivyo, amesema ugonjwa huo hakuwa nao muda mrefu, ulimuanza siku tatu zilizopita kwa homa na kifua, lakini juzi ndiyo ulizidi.
Jerome Rwanda ni msaidizi binafsi wa Membe amesema kabla ya taarifa ya msiba walikuwa pamoja na mwanasiasa huyo saa sita usiku kwa mazungumzo mbalimbali.
Amesema muda huo hakuwa na ishara yoyote ya kuugua zaidi ya kikohozi tena hakikuwa kikali kiasi cha kutishia uhai.
"Nilikuwa na mzee leo (jana) saa sita usiku, tulikuwa tunazungumza mambo mbalimbali kuhusu maisha, hakuwa anaumwa muda huo, ilikuwa kukohoa kwa kawaida tu," amesema.
Kwa mujibu kwa Rwanda, saa 11 alfajiri alipigiwa simu na mke wa Membe kupewa taarifa ya ugonjwa wake, alikwenda na kumpeleka Hospitali ya Kairuki iliyokuwa jirani na eneo hilo.
"Nilipopigiwa niliambiwa anapata shida ya kupumua kwa hiyo nikaenda tukampeleka hospitali," amesema.
Walipofika, amesema Membe aliwekewa kifaa cha usaidizi wa kupumua na baadaye chumba maalumu cha wagonjwa mahututi.
Wakati anasubiri nje ya hospitali hiyo, saa moja asubuhi, amesema aliitwa na mmoja wa madaktari akitawakiwa kuingia ndani.
Amesema baada ya kuingia ndani ndipo alipopewa taarifa ya kufariki kwa mwanasiasa huyo.
Msisitizo kuhusu maisha ndicho, kitakachokumbukwa na Rwanda katika maisha yake ya Membe.
Social Plugin