Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi amewataka wananchi kupuuza kipeperushi kinachosambaa mtandaoni kinachoeleza amesimamishwa uongozi.
Akizungumza na Mwandishi wetu, Ntobi amesema : "Taarifa hizo sina hakika nazo mpaka sasa, kwani sijapata barua rasmi kutoka kwa yeyote Kanda wala Taifa. Nimeona kwenye mitandao ya kijamii kipeperushi chenye taarifa kwa umma. Ninachofahamu nilitegenezewa mashtaka ya uongo na uzushi ili kuchafua na kushusha heshima yangu na zaidi sikupata nafasi ya kusikilizwa".
"Hizi ni ajali za kisiasa zinazotengenezwa tu na hata Mwl Nyerere alitengenezewa na wakoloni, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na wanasiasa wengi tu hutengenezewa zengwe. Kwa sasa niwatake viongozi na wanachama wa CHADEMA Shinyanga kuendelea kuwa watulivu na waamini bado nipo imara sana kuliko jana. Naamini CHADEMA ni taasisi imara nikipata barua rasmi nitaweza kuzungumza na Wana Shinyanga, wanaChadema na Watanzania wote kwa ujumla.
Kwa sasa sina maoni mazuri kuhusu hili kwa sababu sifahamu hata ni kifungu gani cha Katiba yetu kinachotamka adhabu kama hiyo",amesema Ntobi.
Katika taarifa hiyo inayosambaa mtandaoni, Kamati tendaji ya CHADEMA Kanda ya Serengeti imemsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi kutokana na makosa ya nidhamu.
Hata hivyo Katibu wa Kamati ya Uenezi CHADEMA Kanda ya Serengeti, Golden Charles Marcus amesema :
"Taratibu za chama zinampa nafasi mhusika kukata rufaa ya ndani ya siku 30 ,Ntobi ni mwanasiasa mkongwe anajua hatua zote za kuzingatia kuhusu rufaa yake na ana tambua yote juu ya barua hiyo kwa kuwa vikao halali alishirikishwa hadi hatua ya mwisho ya barua hiyo kutolewa na uongozi wa CHADEMA".
Taarifa inayosambaa mtandaoni
Social Plugin