Polisi jijini Kampala nchini Uganda wamewakamata maafisa kumi wa polisi kwa tuhuma za shilingi milioni 5.4 pesa za Kenya kutoka kwa wezi walioiba shilingi milioni 15.
Wanaume watatu waliokuwa kwa pikipiki walimpokonya raia mmoja wa Burundi begi lililokuwa na pesa hizo eneo la Makindye, jijini Kampala.
Raia huyo wa Burundi ambaye alikuwa na pesa hizo kwa sarafu za dola za Marekani na Euro alizimia baada ya kupokonywa begi lake akitoka ofisi ya kubadili sarafu.
Wahisani walimsaidia kurejea kwa miguu yake kabla ya wahisani wao hao kupigia simu maafisa wa polisi kuhusu tukio hilo na maafisa wa kituo cha Polisi cha Katwe kuanza oparesheni.
Inaarifiwa kuwa bila kuwajulisha wakubwa wao wala kuandikisha oparesheni hiyo kwa mujibu wa kanuni, maafisa hao waliwakamata washukiwa eneo la Masajja taarafa ya Makindye.
Maafisa hao walipata pesa hizo na kuwatia mashukiwa katika seli kisha sasa wakaamua kuelekeza kesi kwa wenzao wa Idara ya Upelelezi wa Jinai.
Mambo yalikuwa sawa hadi pale ambapo washukiwa waliambia majasusi kuwa maafisa waliowakamata walisema kiwango kidogo kuliko walichowapata nacho.
Maafisa hao walishikwa mara moja na kufungiwa katika kituo cha polisi cha Katwe ambako walikuwa wamewafungia washukiwa wa wizi waliowashika Makindye.