RAFIKI SDO YAFUNGUA OFISI MPYA MSALALA KUSAIDIA VIJANA WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU



Na Nyamiti Alphonce Nyamiti - Kahama


Shirika lisilo la kiserikali la Rafiki SDO la Mkoani Shinyanga limefungua Ofisi zake katika kijiji cha Kalole kata ya lunguya halmashauri ya Msalala Mkoani Shinyanga itakayowawezesha vijana wanaoishi katika mazingira magumu kujikwamua kiuchumi.

Hafla ya ufunguzi wa Ofisi hiyo umefanyika Mei 19 ,2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kata na halimashauri hiyo huku jamii ikitakiwa kutambua mchango wa shirika kwa kuhakikisha wanapeleka watoto wao kupatiwa elimu ya ujuzi mbalimbali kama vile ushonaji ususi mapambo na vitu vingine.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bwana Giringai Osward Mahemba ambaye ni kaimu mkuu wa divisheni ya Maendeleo ya jamii (W), ameyataka mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikari hususani yanayojishughulisha na kuwakwamua kiuchumi watu walio katika mazingira magumu kuwekeza katika halmashauri hiyo na kuzingatia kitaala ya elimu inayotolewa na serikali.

Hata hivyo Mahemba amesema wao kama serikali wamekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanapiga vita ajira za watoto hususani wale wanaoishi karibu na migodi kutokana na kuwepo Kwa   hali ya watoto kutumikishwa.

"Sisi kama serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tumekuwa tukifanya jitihada kubwa kuhakikisha tunatokomeza ajira za watoto hasa kwenye mazingira ya migodi kama hapa mgodi wa Nyangalata",alisema Mahemba.

Naye Diwani wa kata hiyo Mhe. Bernadict Manuary Amesema uwepo wa kituo hicho kwenye kata yake kutasaidia vijana wengi walio shindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali.

" Tuwapongeze Shirika la Rafiki SDO kwa kazi zenu ambazo mmekuwa mkizifanya kwenye maeneo mbalimbali leo hii kufika kwenu hapa kutasaidia vijana walio wengi kutengeneza fursa za ajira na mimi kama diwani na kamati yangu ya Maendeleo  kata tutakuwa bega kwa bega kuhakikisha tunafikia malengo" ,alisema Manuary.

Kwaupande wake Mratibu wa Mradi  bi Queen Gerald Amesema kwakipindi cha mwaka mzima shirika kupitia wafadhili wa Mradi huo wanaojulikana kama YEP I watawezesha wakufunzi wote watakaojitokeza kwa kuwagharamikia gharama zote za mafunzo kwa asilimia 100.

Baadhi ya wanufaika wa Mradi huo kupitia shirika hilo, Pascazia Joseph na Hulda Joseph wamesema uwepo wa shirika la Rafiki SDO wanatarajia kupata ujuzi utakao wawezesha kujiajiri Ili kujikwamua kwenye changamoto mbalimbali.

" Sisi kama vijana tulikuwa tumeajiriwa kwenye hoteli za mama lishe kuosha vyombo na wengine kwenye maduara kuvunja nawe sàsa tutapata ujuzi wetu kupitia shirika na tutaweza kujiajiri wenyewe", walisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post