MCHAKATO WA KUREKEBISHA SHERIA YA NDOA 1971, WADAU WASISITIZA MIAKA 18


Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Damas Ndumbaro akifungua mkutano wa kujadili Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Damas Ndumbaro akifungua mkutano wa kujadili Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Damas Ndumbaro akifungua mkutano wa kujadili Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
Bi. Anna Kulaya Mratibu wa Taifa wa WILDAF akitoa neno la ukaribisho
Baadhi ya Wabunge walioshiriki mkutano huo
Mwendeshaji wa kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE Rose Ngunangwa Mwalongo akizungumza 
Mwendeshaji wa kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE Rose Ngunangwa Mwalongo akizungumza 
Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Damas Ndumbaro (wa nne kushoto) akiwa na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wanamtandao wa kupinga ukatili jijini Dodoma.

Na Mwandishi wetu - Dodoma
Wadau wamependekeza umuhimu wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Elimu ili kiwango cha chini cha mtoto kupata elimu kuwa kidato cha nne ili kuwalinda watoto na ndoa za utotoni.

Sambamba na hilo, Bunge lifanye marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na kuweka umri wa chini wa mtoto kuolewa kuwa miaka 18.

Wito huu ulitolewa hivi karibuni kama sehemu ya maazimio jijini Dodoma kwenye mkutano uliowakutanisha wabunge wa Jammhuri ya Muungano wa Tanzania na mtandao wa kupinga ukatili Tanzania ili kujadili umuhimu wa kurekebisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Mkutano huo uliandaliwa na WILDAF kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria.

MAAZIMIO YA MKUTANO HUO

Wadau wameshauri umuhimu wa kuijengea uwezo RITA ili iwe na mifumo mathubuti ambayo itasajili ndoa kwa namna ambayo wataweza kutambua ndoa zote zinazofungwa ikiwemo zinazohusisha watoto.

Mojawapo ya maazimio hayo ni pamoja na kuja na mikakati mahsusi ya kutokomeza mila na desturi zilizopitwa na wakati na zenye madhara kama ukeketaji kutokana na kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea ndoa za utotoni.

Mbunge wa viti maalumu Mh. Sophia Mwakagenda alisema kuwa marekebisho ya Sheria ya Elimu hususani kuweka umri wa miaka 18 kama ukomo utasaidia kutokomeza ndoa za utotoni.

Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalumu Mh. Salome Makamba alisema mitaala mipya ya elimu inayopendekezwa itasaidia kutatua changamoto juu ya ndoa za utotoni.

Mbunge huyo alisisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha harakati zote za kumkomboa mtoto wa kike zinakwenda sambamba na kufanya hivyo pia kwa mtoto wa kiume kwani nao pia wanakabiliana na changamoto.

MADHARA YA MTOTO KUOLEWA KATIKA UMRI MDOGO

Mratibu wa WILDAF kitaifa Bi. Anna Kulaya anatoa wito wa Bunge kurekebisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili kuwaokoa watoto na ndoa za utotoni na vifo vinavyotokana na uzazi kwani miaka 14 na 15 ni umri mdogo mno kwa mtoto hususani wa kike kuingia kwenye uzazi na malezi.

Ndoa za utotoni pia zinawanyima wasichana haki ya kupata elimu na kuwatokomeza kwenye dimbwi la ukatili wa kijinsia na umasikini uliokithiri kwani huwa hawana maamuzi na hawana uwezo wa kujilinda kutokana na umri wao kuwa mdogo.

Kwa mujibu wa Kulaya, takwimu duniani zinaonyesha kuwa nchi nyingi zenye viwango vya juu vya ndoa za utotoni ndizo zinazoongoza kwa vifo vya uzazi.

"Nchini Tanzania, takwimu zilizopo kwenye Utafiti wa Kidemographia na Afya wa mwaka 2022 zinaonyesha kuwa vijana walio chini ya miaka 20 wanachangia asilimia 20 ya vifo vya uzazi huku wasichana kati ya miaka 15-24 wakichangia takribani asilimia 40 ya vifo vya uzazi nchiini", alisema Kulaya.


UHALALI WA MIAKA 18 KUWA UMRI SAHIHI KISHERIA

Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inakinzana na sheria nyingine nchiini inapokuja kwenye umri kwani inaruhusu ndoa kwa mtoto wa kike kuanzia umri wa miaka 14 hadi 15 umri ambao mtoto anatakiwa si tu kuwa shuleni bali ni umri mdogo sana kwake kuchukua majukumu ya ndoa na kuanzisha familia.


Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inakinzana na:

👉 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ambapo Ibara ya 5 inampa mtu mwenye umri wa miaka 18 kupiga kura.

👉 Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambapo kifungu namba 4(1) kinatamka bayana kwamba mtu yoyote mwenye umri chini ya miaka 18 ni mtoto.

👉 Sheria ya Uchaguzi katika kifungu cha 342 inatoa haki ya kupiga kura kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 na kutoa katazo kwa mtu wa chini ya umri huo.

👉  Hivyo ni dhahiri kwamba sheria hizo zote nyingine zinatambua kwamba mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 bado ni mdogo mno kufanya maamuzi ya muhimu ambayo kwa vyovyote vile hayawezi kuzidi uzito wa ndoa na uzazi, masuala ambayo yana changamoto nyingi mno.


Hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Damas Ndumbaro alinukuliwa akisema mchakato wa kurekebisha sheria hiyo ulitokana na amri ya Mahakama ya Rufaa ambapo tayari wadau mbalimbali wametoa maoni ya namna ya kuboresha sheria hiyo.


MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post