AMEND, POLISI WATUMA UJUMBE KWA MADEREVA KUELEKEA WIKI YA USALAMA BARABARANI KIMATAIFA,WASEMA AJALI ZINAEPUKIKA

Mmoja wa madereva na Mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam akiwa kwenye Mahakama ya Watoto baada kuvunja sheria za usalama barabarani kwa kutosimama eneo la kivuka vha waenda kwa miguu lililopo eneo la Shule ya Msingi Kisiwani leo Mei 9,2023.Mahakama hiyo ya Watoto inaendeshwa na wanafunzi wa shule hiyo ambao wamepatiwa mafunzo maalum ya kuelimisha jamii umuhimu wa kuzingatia sheria za barabarani.

**************

KATIKA kuelekea katika Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani Kimataifa Shirika la Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wametuma ujumbe kwa madereva nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha vifo na ulemavu wa kudumu miongoni mwa Watanzania.

Wametoa ujumbe huo leo Mei 9,2023 katika Shule ya Msingi Kisiwani wilayani Kigamboni wakati wa utoaji wa elimu ya usalama barabarani kupitia Mahakama ya Watoto ambayo imeratibiwa na Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani.

Neema Swai ambaye ni Meneja Programu wa Shirika lisilo la kiserikali la Amend amesema kwa sasa wanaendelea na utafiti wa kisayansi kubaini elimu ya usalama barabarani inayotolewa kwenye programu ya Mahakama Kifani kama imekuwa chachu ya kupunguza ajali kwa kiwango gani.

Huku akisisitiza matarajio yao ni kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inafika katika maeneo mengi ya shule kwani tangu programu hiyo imeanza imekuwa na mafanikio.

“Shirika letu la Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani tumekuwa tukitoa mafunzo kuhusu elimu ya usalama barabarani kwa kuwakumbusha madereva na watumiaji wengine wa barabara kwamba wakifuata sharia tunaweza kupunguza ajali kwa kiwango kikubwa.

“Hivi sasa tunaelekea kwenye Maadhimisho ya Wiki ya usalama barabarani kimataifa na sisi kama Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tunao wajibu wa kutoa elimu kwa vitendo kupitia program ya Mahakama Kifani kupitia wanafunzi ambao wamepata elimu hiyo na sasa wanapeleka ujumbe kwa jamii,”amesema Swai.

Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi katika Makao Makuu ya kikosi cha Usalama Barabarani Faustina Ndunguru amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na watumiaji wa vyombo vya moto hususan madereva kutozingatia sharia za usalama barabarani.

“Tunaelekea wiki ya usalama barabarani duniani, hivyo Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani kwa kushirikiana na Amend tumeamua kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi ikiwemo Shule ya Msingi Kisiwani.

Ameeleza lengo ni kuwakumbusha madereva kuzingatia sharia za usalama barabara hasa maeneo ya shule ambayo kunakuwa na idadi kubwa ya watoto waovuka barabara.

“Huwa tunasema barabara inaongea maana dereva anapokuwa anaendesha gari kila kitu kinamuelekeza , kama kuna eneo la wavuka kwa miguu ataona alama, kama kuna kona, au ni eneo la kuvuka wanyama lazima utaona alama, lakini hata mwendo gani wa kutembea upo kwenye vibao, hivyo madereva wahahakikishe wanafuata sharia,”amesema Ndunguru

Amesisitiza Tanzania bila ajali inawezekana, hivyo madereva watimize wajibu wao huku akitumia nafasi hiyo kueleza Mahakama ya Watoto imekuwa na mafanikio makubwa kwani kupitia elimu ambayo wanafunzi wameipata wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuhoji madereva wavunja sharia na kuchukua hatua.

Wakati huo huo Wakili Salome Masaga amesema kuwa amefarijika kuona jitihada zinazochukulia na wadau hao katika kutoa elimu na kwamba kumekuwepo na ajali nyingi za barabarani ambazo nyingi zinatokana na madereva kutofuata sharia za usalama barabarani.

Awali baadhi ya madereva ambao wameshiriki katika utoaji wa elimu hiyo kupitia Mahakama ya Watoto wameeleza namna ambavyo elimu hiyo inapaswa kuendelea kutolewa kwa madereva ili watembea kwa miguu hasa wanafunzi kwenye maeneo ya shule wanakuwa salama.

Dereva Babaji anayefanya safari zake kati ya Feri na Kisiwani wilayani Kigamboni Emmanuel Masimo amesema kitendo cha kushindwa kusimama eneo la wavuka kwa miguu na kupelekwa kwenye Mahama ya Watoto amejisikia aibu lakini imempa somo kwamba lazima sharia ya barabarani izingatiwe, hivyo atakuwa balozi mzuri kwa madereva wenzake.

Kwa upande wa Mkazi wa Kigamboni Paul Makanja amesema kitendo Cha wanafunzi kuwa na uelewa mpana kuhusu sheria za barabarani itasaidia kupunguza ajali za barabarani huku akitumia nafasi hiyo kueleza Iko haja ya elimu ya usalama barabarani kuwafikia watu wengi zaidi na hiyo ni njia mojawapo.

Nao wanafunzi wa Shule ya Msingi kisiwani Maria Chacha, Saimon Abdallah na Nuru Issa waliokuwa sehemu ya mahakimu katika Mahakama ya Watoto wameeleza ujumbe wao mkubwa kwa madereva wanawaomba wanapopita maeneo ya shule wazingatie sharia, za usalama barabarani kwani wanafunzi ni watoto wao.

Wamesema madereva wengi waliofikishwa Mahakama ya Watoto wamejisikia aibu kutokana na kuhojiwa na wanafunzi lakini wanaamini madereva hao watakuwa mabalozi wazuri wa kupeleka elimu kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post