Na Saleh Lujuo, Dodoma.
SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) limeandika historia kwa kusaini mkataba wa kuzalisha umeme jua wenye thamani ya Bilioni 274.76 Kwa kutumia teknolojia ya "Solar Photo Voltaic"Wenye uwezo wa kuzalisha megawatt 150 za umeme.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande amesema hayo Jijini hapa leo Mei 29,2023 kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba wa kwanza wa umeme nchini wa kuzalisha umeme wa jua wa megawati 50 Kishapu -Shinyanga mara baada ya kushudia utiaji saini huo baina ya TANESCO na Kampuni ya SINOHYDRO CORPORATION kutoka nchini China.
Amesema mradi huo utatekekezwa kwa awamu mbili ambapo kwa awamu ya kwanza zitazalishwa megawati 50 na awamu ya pili itahusisha uzalishaji wa megawati 100.
Amesema mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya Sinohydro Corporation kutoka China ambapo gharama za mradi hadi ukamilike ni jumla ya shilingi bilioni 274.76 itakayohusisha ulipaji fidia Kwa watakaopisha eneo la mradi.
"Huu ni mradi mkubwa kuwahi kutokea kuzalisha umeme Kwa kutumia nishati ya jua hapa nchini na Katika ukanda wa Afrika mashariki,tunapaswa kujivunia,"amesema Mkurugenzi huyo.
Chande amesema kusainiwa kwa mradi huo ni sehemu ya mpango wa Mapinduzi katika uzalishaji wa umeme Kwa kutumia vyanzo mseto katika sekta ya nishati nchini ili kufikia lengo la kuwa na megawati 5000 kwenye grid ya Taifa ifikapo 2025.
Naye Waziri wa Nishati,January Makamba akiwa shuhuda wa makubaliano hayo ametumia nafasi hiyo kulitaka Shirika hilo(TANESCO), kufanya utafiti na kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo yanayoweza kujengwa miradi ya umeme wa jua na upepo kabla ya fedha za miradi kupatikana .
Waziri huyo amesema kuwa kutokufanya upembuzi na tafiti mapema kunasababisha miradi kuchelewa kuanza kutekelezwa kutokana kutafuta maeneo baada ya fedha kupatikana.
Amesema kuwa ili kwenye gridi kuwe na umeme wa uhakika inatakiwa kuwe na umeme wa aina zote yaani umeme wa jua,upepo,gesi na maji ili ukikwama sehemu moja basi umeme mwingine ufanye kazi.
Aidha Makamba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha washirika wa maendeleo wa Ufaransa(AFD) na Serikali ya Ufaransa ambao ndiyo wafadhili wa mradi huo kwa kumuamini na kuikopesha Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 274.76 kwajili ya mradi huo.
"Tunamshukuru Rais kwakuhakikisha washirika wa maendeleo wa ufaransa na serikali ya ufaransa inamuamini na kutupatia mkopo wa fedha hizo za mradi na ni mkopo wa awamu na awamu ya kwanza ndiyo utakamilisha ujenzi wa hizo megawati 50,"amesema.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla kuhakikisha wanautunza mradi huo kwani unapita katika eneo kubwa la ekari 1000 hivyo siyo rahisi kuliwekea uzio eneo lote.
Pamoja na hayo amesema kuwa mambo yakikaa vizuri Serikali inampango wa kuzalisha umeme jua na umeme upepo katika mkoa wa Dodoma ambapo utazalishwa Zuzu umeme wa upepo megawati 60 .
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Juni 2023 ambapo utachukua miezi 14 hadi kukamilika kwake chini ya ufadhili wa Mashirika ya maendeleo ya Ufaransa (AFD).