Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watumishi watatu wa Shule ya Sekondari Kisomachi, iliyopo Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro kwa uchunguzi wa tukio la vifo vya wanafunzi wawili wa kidato cha nne wa shule hiyo.
Watumishi hao wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa ni mkuu wa shule hiyo, mwalimu wa zamu pamoja na mtunza stoo wa shule hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simoni Maigwa imesema wanafunzi hao walifariki dunia Mei 12 shuleni hapo baada ya kuingia ndani ya tenki la kuhifadhia maharage baada ya sehemu ya chini ya kutolea maharage kuziba.
Wanafunzi waliofariki dunia ni Edson Gabriel Mosha (17) na Godwin John (17) ambao wote ni wanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo.
"Wanafunzi hawa baada ya kuingia kwenye tenki kwa lengo la kutoa maharage kwenye tenki hilo baada ya sehemu ya chini inayotolea maharage kuziba, kwa hiyo baada ya kuingia ndani walikosa hewa na baada ya kutolewa walikimbizwa kituo cha afya Kirua Vunjo ambao ilibainika wameshafariki," amesema.
Miili ya wanafunzi hao imehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Mawezi kwa uchunguzi zaidi.