Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Mei 9,2023 kuelekea Siku ya Kongamano la Sera na Mitaala ya Elimu litakalofanyika kuanzia Mei 12 hadi 14 Mwaka huu katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Mei 9,2023 wakati akizungumza kuelekea Siku ya Kongamano la Sera na Mitaala ya Elimu litakalofanyika kuanzia Mei 12 hadi 14 Mwaka huu katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,wakati akizungumza leo Mei 9,2023 kuelekea Siku ya Kongamano la Sera na Mitaala ya Elimu litakalofanyika kuanzia Mei 12 hadi 14 Mwaka huu katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imeamua kutoa rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na rasimu ya Mitaala Mipya ya Elimu ya Awali, Msingi,Sekondari na Vyuo vya Ualimu hadharani ili kupata maoni ya wananchi.
Hayo yamesemwa leo Mei 9,2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea siku ya Kongamano la Sera na Mitaala ya Elimu litakalofanyika kuanzia Mei 12 hadi 14 Mwaka huu katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Prof. Mkenda amesema mchakato huo umekamilika kwa kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembelea nchi mbalimbali na kufanya uchambuzi.
"Kazi hii imekuwa ikifanyika kwa kukusanya maoni, kutembelea nchi mbalimbali na kufanya uchambuzi wa kitaalamu, ninayo furaha kuwajulisha kuwa rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 toleo la 2023 imekamilika.
"Rasimu za mitaala ya elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu ambayo inakidhi maelekezo ya Rais wetu nayo imekamilika, Serikali imeamua kutoa rasimu hizi ili kupata maoni ya mwisho ambayo tunataka yawe yashapokelewa ifikapo 31 Mei 2023," ameeleza Prof. Mkenda.
Hata hivyo amefafanua kuwa rasimu hizo sasa ziko hadharani ili kupata maoni ya mwisho na zinapatikana katika tovuti za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz), Idara ya habari Maelezo (www.maelezo.go.tz) na ile ya Taasisi ya Elimu Tanzania (www.tie.go.tz).
Ameongeza kuwa “Mei 10, 2023 Wizara itafanya semina na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwapitisha katika rasimu hizo na Mei 12 hadi 14 tutafanya kongamano kubwa la kitaifa la siku tatu la kujadili rasimu hizo."
Prof. Mkenda amewakaribisha wadau wote kujisajili ili kushiriki katika kutoa maoni yao pia amebainisha kuwa mwisho wa kupokea maoni yao ni Mei 31, 2023 baada ya hapo rasimu hizo zitapelekwa katika ngazi za maamuzi mwezi Juni, 2023.
“Haya ni mageuzi makubwa sana katika elimu yetu na kalenda ya awamu ya utekelezaji wa mambo yatakayoingizwa katika mitaala hiyo ambapo itaamuliwa nini kifanyike mwaka huu, nini kifuate na tunamaliza na kipi” amesisitiza Mkenda
Aidha amesema kuwa kesho watafanya semina kwa wabunge wote ili wazipitie rasimu na kwamba Kongamano la Kitaifa litafanyika kwa siku tatu kujadili rasimu hizo ambapo wanaotaka kushiriki watajisajili kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya wizara hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kongamano hilo ni la kimataifa na wamewashirikisha watanzania wanaoishi nje ya nchi ili kutoa maoni yao na uzoefu wao katika nchi wanazoishi.
“Kongamano hili ni la Kimataifa tumeshirikisha watanzania wanaoishi nje ya nchi ili nao watupe uzoefu wao katika nchi wanazoishi katika kuboresha mitaala yetu” amesema Prof .Nombo.
Social Plugin