Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI WARIDHISHWA NA KASI MIRADI YA KUSAMBAZA MAJI


Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga-(SHUWASA) wameridhishwa na kasi ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na mamlaka hiyo ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi ambao hawajafikiwa.

Akizungumza mara baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya usambazaji wa majisafi katika maeneo ya Didia na Tinde, Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Joyce Egina, amesema wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imepata fedha kutoka wizara ya maji na inatarajia kukamilika miezi michache ijayo.


“Tumekuja kutembelea miradi mbalimbali tukianzia Didia hadi Tinde na huu mradi wa Tinde ni mradi ambao maendeleo yake ni mazuri, hivyo basi ili kuhakikisha mradi unakwenda vizuri na mkandarasi anafanya kazi ndani ya muda aliopewa, sisi kama wajumbe tumefurahi kwasababu mradi wetu umeanza mwezi wanne na leo unakaribia kukamilika,” amesema na kuongeza;


“Tumeamua kufanya ziara ili kujiridhisha na kuona mradi unakwendaje ili wanachi wetu wapate maji kwa wakati kwasababu ni mradi ambao umefadhiliwa na Wizara ya Maji hivyo basi tunatumaini baada ya muda mfupi vijiji vilivyopo jirani na eneo hili vitakuwa vimepata maji.”


Naye mjumbe wa bodi hiyo ambaye ni mwakilishi kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Ramadhani Singano, amesema wameshuhudia miradi ya ujenzi wa matangi mawili katika miji ya Didia na Dandugu ambayo amebainisha kuwa yote imefikia asilimia 99 na inatarajiwa kukamilika hivi karibuni na wananchi kuanza kupata huduma ya maji safi.

Aidha amesema wametembelea mradi wa kusambaza mtandao wa maji katika vijiji vitatu vya mji mdogo wa Didia na kuridhishwa na kasi ya mkandarasi licha ya kuwepo kwa changamoto ya miamba ambayo inahitaji kulipuliwa.

Akitoa maelezo kuhusu miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, CPA Sarah Emannuel, aliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kupitia Wizara ya Maji.


Amesema miradi hiyo inaendelea vizuri licha ya changamoto ya upasuaji wa mawe na kwamba menejimenti ya SHUWASA inaendelea kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo ikiwemo kuangalia sheria inasemaje kuhusu suala hilo.


Amesema mradi huo utafikisha maji kwa takribani wananchi wa vijiji vitatu vya Tinde na tathimini inaendelea kwaajili ya kufikisha maji vijiji vingine kikiwemo kijiji cha Buchama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com