Serikali imesema kuwa maonesho ya elimu yanayolenga kuunganisha Vyuo vya ufundi, juhudi za ubunifu, sayansi na teknolojia pamoja na shughuli za uzalishaji kuanzia sasa yatakuwa yakifanywa kwa pamoja.
Hayo yamesemwa na Waziri w Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Mei jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Pili ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yanayoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET)
Prof. Mkenda ameongeza kuwa kuunganishwa kwa maonesho hayo kutasaidia wananchi kupata taarifa na huduma za elimu kwa wakati mmoja pamoja na kuwakutanisha waajiri na vyuo vinavyotoa mafunzo ili kuweza kufahamu soko la ajira linataka nini.
"Tutahakikisha maonesho haya yanaunganisha Vyuo vya ufundi, juhudi za ubunifu, sayansi na teknolojia pamoja na shughuli za uzalishaji na huduma kwa ajili ya kutengeneza uwezo wa kutambua mahitaji na kuimarisha utoaji mafunzo kwa vitendo kwa vijana wetu," amesema Prof. Adolf Mkenda.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Husna Sekiboko ameishukuru Wizara kwa kuishirikisha Kamati hiyo katika shughuli zote za Wizara na kuahidi kwamba itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mageuzi makubwa ya elimu yanayotarajiwa yanatokea.
Akizungumzia maonesho ya NACTVET Makamu Mwenyekiti huyo amesema kuwa maonesho hayo ni mazuri huku akiwataka wananchi kujitokeza kuona namna kazi kubwa ya ubunifu na ufundi zinazofanyika katika Vyuo na Taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya ufundi.
Naye mmoja wa wadhamini Deogratius Haule kutoka Geita Gold Mine amesema wataendelea kudhamini maonesho hayo ili vijana wa Vyuo vya kati na Taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo zipate fursa ya kuonyesha uwezo, vipaji na ubunifu wanaofanya na hivyo kuleta maana halisi ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu la Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt Adolf Rutayuga amesema kuwa nchi nyingi Duniani zinatambua kuwa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda, hivyo inapaswa kuzingatia umahiri wa kutenda na mahitaji ya soko la ajira kwa wahitimu.
Ameongeza kuwa ili kuwepo na elimu yenye tija inayojibu changamoto za jamii ni lazima kuwepo kwa ushirikiano kati ya watoa mafunzo na waajiri.
Maonesho ya Pili ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yanayoendelea jijini Arusha yameshirikisha zaidi ya Taasisi 200 zikiwa ni Vyuo vya elimu ya ufundi, ufundi stadi, Vyuo vikuu, Taasisi na Makampuni ya waajiri, wajasiliamali na vikundi mbalimbali vinavyofaidika na elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Social Plugin