MAIPAC YABAINI WATOTO WADOGO KUKEKETWA KWA SIRI LONGIDO

 

 Mary Laizer Muelimishaji Jamii Longido.


MAIPAC yabaini watoto wadogo kukeketwa kwa Siri Longido.

Mwandishi wetu, Longido

maipacarusha20@gmail.com

Shirika la wanahabari wanaosaidia Jamii za pembezoni (MAIPAC) limebaini uwepo wa matukio ya ukeketaji kwa watoto waliochini ya miaka mitano wilayani Longido mkoa wa Arusha.

Baadhi ya wazazi wa Jamii ya kifugaji katika Wilaya hiyo,wameanza kuwakeketa watoto wakiwa wachanga ili kukwepa kukamatwa na vyombo vya dola.

Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari wanachama wa MAIPAC wanaofanya uchunguzi juu ya kuibuka matukio ya ukeketaji watoto ,Wilaya ya Longido mkoa wa Arusha,baadhi ya wazazi na maafisa wa serikali wilaya ya Longido walisema bila hatua kali kuendelea kuchukuliwa ukatili huu dhidi ya watoto hautakoma.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo ambayo asilimia 95 ya wakazi ni wafugaji wa Jamii kimasai wameeza kuwa kutokana na jitihada na serikali wilaya Longido kudhibiti watoto wakiwa shuleni kufanyiwa ukeketaji baadhi ya wazazi sasa wanakeketa watoto wachanga.

Paulo Orkediaye mkazi wa Kijiji Cha Oltepesi anasema licha ya elimu kuendelea kutolewa baadhi ya wazazi wanakeketa watoto wachanga kwa Siri.

"Hi tabia ni mbaya Sana tunatoa elimu kupinga ukeketaji lakini baadhi ya wazazi wanaendelea"alisema

Neema Nailom mkazi wa Olbomba alisema mkakati wa kukeketa watoto wachanga unafanywa kwa uficho baina ya mama mzazi na baadhi ya Ngariba.

"Huwezi kubaini mapema kwani ni Siri wanafanya sisi tunawabaini watoto pale ambapo wanaumwa na kupelekwa Hospitali"alisema

Jane Melei mkazi wa Kimokowa alisema mzazi wake alimkeketa mdogo wake akiwa mdogo kutokana na Mila hiyo kuendelea na kutaka mtoto awe na heshma ya kuolewa.

"Hata Mimi nimekeketwa nikiwa mdogo lakini wazazi walifanya hivi ili niwe na hadhi ya kuolewa maana huku kwetu Kama hujakeketwa ni ngumu kupata mtu wa kukuoa"alisema.a

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Longido,Grace Mghase amesema kuendelea kwa vitendo vya ukeketaji vinachangiwa na vijana kuwa wazito kuoa binti ambaye hajakeketwa.

"Hili Jambo bado linamizizi Sana sisi tunatoa elimu lakini ajabu kuna vijana na wasichana wenye elimu lakini bado wanaunga mkono ukeketaji"alone

Grace alisema hata baadhi ya wanasiasa katika Wilaya hiyo bado wanaogopa Mila hi potofu kuipinga hadharani.

"Ni kweli tunataarifa wanakeketa watoto wachanga ili kukwepa kukamatwa lakini wajuwe serikali ina mkono mrefu tukiwabaini watakamatwa"alisema

Merkinoi Orkendiaye alisema vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikiendelea licha ya madhara ikiwepo kuugua ugonjwa wa festula.

"Mimi nilifanyiwa ukeketaji nikipata festula na Sasa nimekuwa natoa elimu kupinga ukeketaji"amesema.

Mary Laizer muelimisha Jamii kupinga ukeketaji Wilaya ya Longido alisema madhara ya ukeketaji ni makubwa ikiwepo kupoteza maisha.

"Mimi mwenyewe nilifanyiwa ukeketaji wazazi wangu Walikuwa hawajuwi athari zake lakini Sasa wamejua na Mimi nimekuwa natoa elimu kupinga ukeketaji"alisema

Alisema hivi Sasa wanahamasisha kuwavusha Rika watoto wa kike bila kuwakeketa lakini pia kutoa elimu kwa vijana kuacha Mila ya kupinga kuoa msichana ambaye hajakeketwa.

Mkurugenzi wa taasisi ya Ewang'ani Maasai Foundation,Nangidare Laizer alisema changamoto ya ukeketaji ni kubwa lakini wanaendelea kutoa elimu .

"Mimi Kama msichana tunakwenda vijiji tunatoa elimu japo kina wazazi wanaendelea kukeketa watoto kwa Siri"alisema

Mkurugenzi wa Shirika la TEMBO la Wilaya ya Longido mkoa Arusha, Pauline Sumayani alisema changamoto ya ukeketaji bado ipo lakini shirika lao linajitahidi kutoa elimu kupinga ukeketaji.

"Tunatoa elimu kwa wanawake,vijana na wazee kuacha ukeketaji na tumekuwa tukitoa zawadi kwa wazazi ambao wanawavusha Rika watoto bila kuwakeketa"alisema

Mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma alisema lengo la kupeleka wanahabari kufaunya uchunguzi huo ambao umedhaminiwa na marafiki wa taasisi hiyo wa nchini Canada ni kukomesha ukatili dhidi ya watoto wa kike katika Jamii hiyo.

"Tumebaini bado elimu inahitajika ya kupinga ukeketaji na elimu inapaswa kuwalenga hata vijana ambao ndio wanachochea ukeketaji kwa kukataa kuwaona wasichana ambao hawajakeketwa"amesema.

Alisema pia wamebaini watoto wachanga kufanyiwa ukeketaji na hivyo kuiomba serikali kupitia maafisa wa afya kufanya uchuguzi kwa watoto wanaofikishwa hospital na wakibaini kufanyiwa ukatili wazazi wachukuliwe hatua.

"Tunawapongeza marafiki wa MAIPAC kwa Nchini Canada kwa kutusaidia kuendelea na uchunguzi juu ya matukio ya ukeketaji Wilaya ya Longido lakini pia kutoa elimu ya kupinga ukeketaji"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post