KATIBU MTENDAJI WA TUME YA MADINI AWATAKA WACHIMBAJI WA MADINI KIGOMA KUWA WAZALENDO

 Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka wachimbaji wa madini mkoani Kigoma kuwa wazalendo na kutokuwa sehemu ya uhujumu uchumi kwa kutorosha madini na kupeleka nje ya nchi kwani vitendo hivyo vinachangia Serikali kukosa mapato yenye kuleta maendeleo nchini.


Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Mei 30, 2023 kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa madini mkoani Kigoma yenye lengo la kuwajengea uelewa zaidi kuhusu usalama, uhifadhi na usimamizi wa mazingira, masuala ya baruti kwa wachimbaji wadogo wa madini sambamba na sheria za madini.


Amesema kuwa, lengo la Tume ya Madini ni kuhakikisha wachimbaji wadogo na wakubwa wa madini wanachangia kwa uwiano sawa wa asilimia 50 kwa 50 katika Pato la Taifa tofauti na asilimia 40 wanayochangia kwa sasa.


Akizungumzia hali ya ukusanyaji wa maduhuli, Mhandisi Samamba amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 lengo la makusanyo lililowekwa na Serikali kupitia Sekta ya Madini lilikuwa ni Shilingi Bilioni 822 ambapo mkoa wa Kigoma ulipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 1.6 kulingana na madini yanayopatikana ambapo hadi kufikia Mei 29 mwaka huu mkoa umekusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3


Katika hatua nyingine, amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanaimarisha mahusiano na jamii inayozunguka migodi yao kwa kuboresha huduma za jamii kama vile maji, elimu, afya, miundombinu kama sheria ya madini inavyotaka.


Aidha, Mhandisi Samamba amewataka wachimbaji wa madini pia kuhakikisha wanachangamkia fursa nyingine za uwekezaji zilizopo kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa kushirikiana na nchi za jirani ikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Burundi ili kuzidi kujiongezea kipato.


Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Chama Cha Wachimbaji Wadogo wa Madini - Kigoma (KIGOREMA) Boazy John amesema kuwa elimu inayotolewa kwenye mafunzo hayo inakwenda kuongeza tija zaidi katika uchimbaji wa madini mbalimbali yanayopatika mkoani humo.


Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na Viongozi wa Mkoa, Kanda, Wilaya pamoja na wachimbaji na wafanyabiashara wa madini mkoa wa Kigoma kutoka katika Wilaya za Kasulu, Uvinza ,Buhigwe , Kibondo na Kakonko.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post