Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MPWAPWA AIFUNGIA SEKONDARI AMBAYO HAINA MWALIMU HATA MMOJA


*Wanafunzi wanalala chini kwenye vumbi, hakuna mkuu wa shule.

*Kuna wanafunzi wanne tu kidato cha nne hawajawahi kusoma Kingereza,Kiswahili

Na Mwandishi Wetu,

MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Sofia Kizigo ametangaza kuifunga Shule ya Sekondari Nelson Memorial kutokana na kubainika kuwepo kwa changamoto mbalimbali zikiwemo za shule kutokuwa na mwalimu hata mmoja mwenye sifa ya ualimu pamoja na kutokuwa na Mkuu wa Shule.

Aidha changamoto nyingine ni uchache wa vitanda vya kulala wanafunzi wa bweni , hivyo wanalazimika kulala chini kwenye sakafu ya vumbi na wengine kulala wawili wawili kwenye kitanda kimoja jambo ambalo haliruhusiwi lakini pia kuna wanafunzi wanne tu wa kidato cha nne ambapo kisheria hawataruhusiwa kufanya mtihani shuleni.

Akizungumza leo Mei 15,2023 baada ya kufika kwenye shule hiyo, Mkuu wa Wilaya Mpwapwa Sofia Kizigo amesema wamelazimika kuifunga kutokana na changamoto lukuki zinazoikabili shule hiyo iliyopo Kata ya Kibakwe iliyopata usajili wake Novemba mwaka 2022 ikiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza.

“Wakati Serikali inafuatilia shule hii kupitia mfumo maalum tuliona kuna wanafunzi wengine wanahamia na hadi leo tunaifunga kulikuwa na wanafunzi 69 ambapo waavulana 39 na wasichana 30, kati yao kulikuwa na wasichana 26 wanaokaa bweni na wavulana 32 , hivyo jumla wanafunzi wa bweni 58.

“Januari 24 mwaka 2023 Mdhibiti Ubora wa Shule wa Mkoa alikuja kutembelea shule na akaagiza wanafunzi kwenye hii shule waondolewe na shule ifungwe kutokana na changamoto ambazo amezikuta na Mei mwaka huu nilipata malalamiko kutoka kwa wasamalia wema walisema mwalimu mkuu anapita mtaani na kurubuni watoto wahamie kwenye shule yake…

“Wakati tunafuatilia tukabaini hiyo shule tangu Januari 24 mwaka huu iliamriwa ifungwe kwani haikidhi vigezo kutokana na changamoto nyingi , hivyo Serikali ikaendeela kufanya ukaguzi na wiki iliyopita tuliagiza shule ifungwe lakini baadae nilipokuja kufuatilia tukakuta wanafunzi bado wapo wanaendelea kusoma.

“Kwa hiyo leo tumekuja kuangalia changamoto na kuifunga rasmi maana tumekuta changamoto nyingi , mfano vitanda vichache na katika bweni la wavulana ambako wako 32 lakini kuna vitanda tisa ambavyo vinaweza kulaza wanafunzi 18 tu.

“Wakati huo huo kumbuka wanafunzi wa bweni wa kiume wako 32 maana yake watoto wengine wa kiume wanalazima kulala na wenzao kwenye kitanda kimoja kitu ambacho sio sawa na marufuku kabisa. Kwenye bweni la wasichana kuna vitanda nane vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 16 peke yake.

“Wengine walikuwa wanakosa vitanda wanalala chini na wengine na walalala zaidi ya mmoja , kitu ambacho hakikubaliki nan i kinyume cha muongozo unaosimamia shule za sekondari.Pia tumeikuta sakafu ya vumbi na watoto wanalala chini kinyume na utaratibu,”amesema .

Ameongeza hata katika upande wa afya za watoto hairuhusiwi kukaa sehemu kama hiyo lakini changamoto nyingine kuna wanafunzi ambao waliofauli vizuri mitihani yao kuna wazazi walisema hawawaoni watoto wao na jirani na hapo kuna shule ya sekondari kwa maana ya wale watoto wenye akili walikuwa wamepelekwa shule nyingine.

“Ikagundulika wanafunzi wameshawishiwa na kuhamia kwenye shule jirani.Ndani ya wiki huwezi kuhamisha watoto ambao wamesajiliwa kufanya mtihani shule nyingine , kwa hiyo walikuwa kama wamedanganywa japo leo tulipokwenda shuleni hapo tumekuta wanafunzi hao wamerudi kwenye shule waliyopo kutokana na maelekezo niliyoyatoa awali.

“Hata hivyo tulipokwenda leo tumekuta kuna wanafunzi wanne wa kidato cha nne na sheria hairuhusu kama shule inawatoto chini ya saba kufanya mtihani , kwa hiyo wanatakiwa kwenda kufanya mtihani sehemu nyingine , kwa hiyo hata hao wanafunzi hawajaambiwa kama hawataruhusiwa kufanya mtihani kwasababu wako wanne tu.

“Pia kuna changamoto walimu kwani tumewakuta vijana sita wa kiume ambao hawajasomea ualimu lakini ndio wanaofundisha wanafunzi , hawana mikataba ya kazi wala sifa za ualimu.Waliosoma ualimu ni wawili tu wengine wamesoma masomo ya sayansi na teknolojia, ufundi umeme na usanifu majengo.”

Amefafanua kwa hiyo vijana hao kwa ujumla wanafundisha masomo ya jiografia , hesabu, fizikia , na Civics na ukiangalia katika shule za sekondari kuna masomo ambayo ni lazima yafundishwe , kuna masomo ambayo mwanafunzia anaweza akachagua.

Amesema kwa mfano wanafunzi wengi wakifika kidato cha tatu wengine wanaamua kuachana na masomo Fizikia na Kemia lakini kuna masomo ya lazima kusoma kama Kingereza na Kiswahili.

“Katika shule hii haifundishi Kingereza wala Kiswahili kwasababu walimu hakuna , kwa hiyo watoto hawajahi kusoma hata siku moja na hiyo ni changamoto nyingine na hao vijana walioajiriwa kama walimu ukweli sio walimu na hawana sifa ya ualimu, hata mikataba ya kazi hawana.

“Kwa hiyo likitokea jambo lolote wanaweza kuruka kwasababu hawana mikataba ya kazi , changamoto nyingine iliyopo shuleni hapo ni wanafunzi wamekatazwa kabisa kuwasiliana na wazazi wao na shule hawaruhusu kukaa na simu na wanafanya hivyo ili wanafunzi wasiseme changamoto zilizopo shuleni na watoto wengi wametokea Dar es Salaam.

“Wamesoma shule kama St.Marry na nyingine za aina hiyo , hivyo walivyofika tu shuleni hapo wakakatazwa kuwasiliana na wazazi wao na hakuna simu kabisa. Kuna mtoto mmoja alifanikiwa kupata simu na akawasiliana na mzazi wake kumueleza mazingira yalivyo kwamba hayafai.

“Mzazi akakasirika akampigia simu mwalimu mmojawapo . Baada mzazi kupiga simu shuleni yule mwanafunzi wakamchukua wakampiga sana kwa kumchangia na wakamwambia kwamba tunampigia mzazi wako na aongee mbele ya walimu wakisikia na awaambie wazazi shule ni nzuri na mazingira ni mazuri.

“Kwa hiyo mtoto akafanyiwa hivyo na wamekuwa wakichapwa sana, pia chakula wanachokula sio kizuri kwasababu watoto wamelalamika wanaumwa sana matumbo halafu hawapelekwi hospitali na chakula ni duni.Lakini huwezi kuwa na shule ya bweni kama huna Matroni na Patroni (walezi) na hao watumishi sita ambao wamesema kama wameajiriwa hao hao ndio ndio matroni na patroni , yaani hao ndio kila kitu.”amesema.

Kizigo ameongeza shule hairuhusiwi kuwepo kama hakuna mkuu wa shule lakini shule hiyo haina mkuu wa shule , aliyojenga hiyo shule ndio mkuu wa shule, ndio mkurugenzi yaani yeye ndio kila kitu na hadi leo hawajafanikiwa kuonana kwasababu anazozijua yeye.

“Tulipofika shule kuna simu tuliyopewa tukazungumza naye , tumekubaliana aje ofisini kwa ajili ya kufuatilia hilo suala na hiyo.”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com