Na.Mwandishi Wetu-Arusha
Katibu mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amezipongeza Taasisi za SOS Children’s Tanzania na Turkish Maarif Schools kwa ubunifu na ushirikiano mkubwa na Serikali katika kuwalea, kuwatunza na kuwapa nafasi za masomo watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu.
Dkt. Jingu ametoa pongezi hizo alipotembelea Taasisi zinazotoa huduma za watoto mkoani Arusha ili kujiridhisha na huduma zinazotolewa kama zinaendana na matakwa ya Serikali.
Ametoa wito kwa uongozi wa Taasisi hizo kushirikiana na Serikali kuendelea kuhakikisha, licha ya kuwa watoto hao ni yatima na wanatoka kwenye mazingira magumu, wanapatiwa malezi bora yanayoendana na maadili ya jamii za Kitanzania na kuongeza kuwa, ikiwezekana huduma zao zitolewe nchi nzima kwa kuwa zitasaidia kupunguza baadhi ya changamoto wanazopitia watoto wa aina hiyo nchini.
“Nimefurahi kuona mnawapa watoto wetu malezi bora kulingana na mila, desturi na tamaduni za Kitanzania, msingefanya hizi ‘intervention’ pengine watoto wangekuwa wanahangaika na kuzurura mitaani bila kuwa na mwelekeo lakini hapa mnawatunza kama familia zao, ubunifu mlioufanya ni jambo la kuigwa, mnachokifanya hapa Arusha, pangeni namna ya kueneza programu hii nchi nzima”. Amesema Katibu Mkuu huyo.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi nyingine zinazoendesha huduma kama hizo kuhakikisha zinafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kuwa na uhakika na huduma wanazozitoa na kuendelea kuwasaidia watoto wa Kitanzania wenye mahitaji kama hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la SOS Tanzania, David Mulongo kwa niaba ya Taasisi hizo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara husika, kwa ushirikiano wanaowapa huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika hatua zote za uanzishwaji wa programu mpya za kuwasaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Shirika la SOS Children’s Center, lililopo eneo la Ngaramtoni, halmashauri ya Arusha, linajishughulisha na kuwasaidia wototo yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu kwa kuwapatia huduma za malezi na makuzi ya kifamilia huku wakipata elimu katika taasisi ya Turkish Maarif Schools.