Shirika la Maendeleo ya Wanawake (Forum for Women and Development- FOKUS) la nchini Norway limeahidi kuendelea kufadhili shughuli zinazotekelezwa na shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI lililopo mkoani Mwanza.
Mshauri wa Programu ya kuwawezesha wanawake kutoka shirika la FOKUS, Joar Svanemyr aliyasema hayo Mei 09, 2023 wakati akishuhudia namna shirika la KIVULINI limekuwa likishirikisha makundi mbalimbali kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto na wanawake katika Wilaya ya Magu.
Svanemyr alisema mbinu zinazotumika na shirika la KIVULINI kuwakusanya wananchi kwenye makongamano mbalimbali ya kuelimisha jamii ikiwemo kuwatumia wanaharakati ngazi ya jamii, bodaboda, wasanii wa ngoma za asili pamoja na mashabiki wa timu za soka za Simba SC na Yanga SC zimekuwa kivutio kikubwa kwake kwani zimesaidia kuleta mabadiliko wilayani Magu.
Akizindua matawi ya timu za Simba SC na Yanga SC katika Kijiji cha Nyang’hanga Kata ya Sukuma wilayani Magu na kukabidhi vyeti kutoka shirika la KIVULINI, Svanemyr alivutiwa na hamasa ya mashabiki wa timu hizo na jumbe walizoziandika kwenye matawi hayo na kuahidi kwamba shirika la FOKUS litaongeza ufhadhili zaidi ili elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ifike katika Kata zilizobaki wilayani Magu kwani kwa sasa ni Kata nne kati ya 25 ndizo zimefikiwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali pamoja na makundi mbalimbali katika jamii kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhamasisha maendeleo ambapo hadi sasa zaidi ya mashabiki 400 wa Simba na Yanga wanasaidia kufikisha elimu hiyo nyumba kwa nyumba.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Lilian Michael alisema vitendo vya ukatili vikitokomezwa katika jamii itasaidia m wenye afya bora, elimu bora na makazi bora ambapo kwa pamoja inasaidia jamii pia kuwa na uchumi imara hivyo malengo ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutosomesha watoto wa kike, vipigo na ndoa za utotoni lazima vitokomezwe.
Nao baadhi ya wanaharakati na mashabiki wa timu za Simba na Yanga wilayani Magu wakiwemo Grace John, Samwel Kaswahili, Veronica Mahingu na Amos Sayi walisema hapo awali kulikuwa na matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini baada ya kuanza kupita kaya kwa kaya kuelimisha jamii, matukio hayo yamepungua na sasa wanafamilia wanashirikiana katika shughuli za maendeleo katika Kata nne za Sukuma, Jinjimili, Kabila na Nyang’hanga ambazo shirika la KIVULINI linatekeleza mradi wa kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kushoto) akitafsiri hotuba ya Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr (kulia) aliyefika Magu mkoani Mwanza kushuhudia mbinu mbalimbali zinazotumika kutoa elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr (kulia) akikabidhi cheti kwa mashabiki wa timu ya Simba SC tawi la Nyang'hanga wilayani Magu kilichotolewa na Shirika la KIVULINI ili kutambua mchango wao wa kuelimisha jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr (wa pili kulia) akikabidhi cheti kwa mashabiki wa timu ya Yanga SC tawi la Nyang'hanga wilayani Magu kilichotolewa na Shirika la KIVULINI ili kutambua mchango wao wa kuelimisha jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Picha ya pamoja na mashabiki wa timu ya Yanga SC tawi la Nyang'hanga wilayani Magu baada ya Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr kuzindua rasmi tawi hilo.
Picha ya pamoja na mashabiki wa timu ya Simba SC tawi la Nyang'hanga wilayani Magu baada ya Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr kuzindua rasmi tawi hilo.
Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr akifurahia burudani na wakati wa Magu.
Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway, Joar Svanemyr na wanaharakati ngazi ya jamii wilayani Magu wanaosaidia kutoa elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Mshauri wa Programu ya Wanawake kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway- Joar Svanemyr (katika), Mkugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI- Yassin Ally (kushoto) na Diwani Kata ya Sukuma ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Magu- Faustine Makingi (kulia).
Mashabiki wa Yanga SC tawi la Nyang'hanga Magu wakifurahia burudani.
Kikundi cha wanawake kikitoa burudani yenye ujumbe wa kuhamasisha jamii kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mashabiki wa Simba SC tawi la Nyang'hanga Magu wakieleza namna walivyosaidia jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mashabiki wa timu ya Yanga SC tawi la Nyang'hanga Magu wakieleza namna wanavyohamasiwha jamii kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia na kujikita kwenye shughuli za maendeleo.
Wanaharakati ngazi ya jamii wakieleza namna wanavyoelimisha wananchi kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Lilian Michael akihamasisha jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hatua itakayosaidia kufikia lengo la Millenium kwa jamii kuwa na afya bora, elimu, makazi bora na uchumi imara.
Tazama Video hapa chini
Social Plugin