Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, imesema katika Mkoa wa Mtwara jumla ya vijana 1,663 wamenufaika na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi.
Kati ya Vijana hao, 891 wamenufaika kupitia mafunzo ya uanagenzi katika fani za uashi, uchomeleaji, ufundi bomba, ufundi magari, ufundi rangi, umeme wa majumbani, umeme wa magari, upishi, useremala na ushonaji.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo ameyasema hayo Mei 18, 2023 alipokuwa akijibu swali Mbunge Viti maalum (CCM) Mhe. Agness Hokororo kwa niaba ya Ofisi hiyo.
Katika swali lake, Mbunge huyo ametaka kujua kwa kiasi gani vijana wa Mtwara wamenufaika na Programu ya Kukuza Ujuzi.
Akijibu swali hilo, Mhandisi Kundo amesema pia vijana 772 wamenufaika na mpango wa urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Kupitia mfumo huo, amesema vijana wamepewa vyeti katika fani za useremala, uashi, ufundi magari, uungaji na uchomeleaji vyuma, ufundi umeme, ubunifu wa mavazi na teknolojia ya nguo, uandaaji na upishi wa vyakula, utandazaji na ufungaji mabomba.
&&&&&
Social Plugin