Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HAKUNA VIFO WALA MIFUGO YA NG’OMBE ILIYOUAWA KIJIJI CHA MWANAVALA- MCHENGERWA


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Zuberi Homela na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi leo wamefika kwenye kijiji cha Mwanavala wilayani Mbarali kutokana na agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa la kuwataka kufika ili kuona hali ya ugomvi uliofanyika mei 6, 2023 baina ya wananchi na wahifadhi pia mifugo liyokamatwa na kuuawa hali ambayo imethibitika kuwa hakuna kifo wala mifugo ilishikiliwa au kuuawa.

Hoja hiyo iliibuliwa jana na Mbunge wa Mbarali, Mhe. Fransis Mtega aliyeomba kutoa hoja ya dharula ya kulitaka bunge lijadili suala hilo hatimaye Waziri Mkuu kutoa maelekezo hayo ambapo leo ujumbe huo ulipata fursa ya kwenda na kukutana waathirika wa tukio hilo na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali na kufika eneo la tukio ambalo limebainika kuwa kilomita 20 ndani ya Hifadhi kwa mipaka ya awali na mita chache na kingo za Mto Ruaha.

“Nimesikitishwa sana na kauli za Mbunge ambapo baadhi ya malalamiko na shutuma zake dhidi ya Serikali zimeleta taharuki kubwa ambayo sijaikuta katika eneo hili na kwamba wananchi wamekiri kuingia ndani ya eneo hili na wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuwatafutia maeneo ya kuishi” amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Ametaja baadhi ya tuhuma ambazo hazina ukweli na ambazo zimethibitishwa na wananchi wenyewe kuwa si kweli ni pamoja na wananchi kukataa kuwa hakuna mifugo iliyochukuliwa na wahifadhi 230 kama ilivyoripotiwa na Mbunge zaidi ya prukushani ya Mbwa wakali wa wananchi husika na wahifadhi, ambapo pia wananchi hao wamekiri kufanya shughuli zao ndani ya Hifadhi na wameomba wananchi hao kuzingatia sharia za uhifadhi hasa Sheria ya TANAPA.

Aidha, amewaonya viongozi wa kisiasa kuacha kuwachonganisha wananchi na serikali yao ambapo amesisitiza kuwa wananchi ni wahifadhi namba moja.

Amemwelekeza Katibu Mkuu wa Maliasili kuchukua hatua dhidi ya askari waliohusika kuwachapa wananchi husika.Ametoa mkono wa pole wa shilingi milioni moja kwa wananchi watano kila moja kama kifuta machozi kwa wahusika.
Kwa upande mwingine Mhe. Mchengerwa amekutana na Uongozi mzima wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbarali ukiongozwa na Mwenyekiti wa Wilaya, Katibu na Makatibu wote wa Kata na Matawi wa CCM Wilaya ya Mbarali na amewaomba waendelee kuwa karibu na wananchi na kutoa elimu ya uhifadhi huku akisisitiza kuwa hifadhi zote ni za wananchi na wananchi ndiyo msingi wa nchi yoyote duniani.

Amesema "Ibara ya 68 ya Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya Mwaka 2020-2025 inasisitiza uhifadhi wa raslimali hivyo sisi sote tunapaswa kushirikiana kwa pamoja tuhifadhi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye" Amefafanua kuwa tatizo la mipaka katika Hifadhi hiyo linakwenda kumalizika ambapo amesema jumatatu anasaini GN mpya ya mpaka wa eneo hilo.

Aidha, amesema mipaka ya Hifadhi hiyo iliwekwa mwaka 1910 wakati Hifadhi hiyo ikijulikana kama Saba Game Reserve na mwaka 1946 ikijulikana kama Hifadhi ya Rungwe na hatimaye mwaka 1964 kama Hifadhi ya Ruaha hadi sasa.
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona kuwa kero zote katika maeneo ya Hifadhi zinatatuliwa kwa amani na upendo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia aliambatana katika ziara hiyo na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, na wilaya ya Mabarali na viongozi wa CCM wa wilaya hiyo aliwaambia wananchi katika mkutano huo kuwa Serikali itahakikisha kuwa wananchi wote wanatendewa haki ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini za makazi na kuwalipa fidia stahiki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com