Halmashauri ya wilaya ya Kibiti mkoani Pwani imeanza kupatiwa Mafunzo ya Sera ya Misitu na Sera ya Ufugaji Nyuki yakilenga kujenga uelewa na kutoa elimu kwa wadau wa misitu ili kuwasaidia wakazi wa wilaya hiyo kufanya shughuli za ufugaji nyuki.
Akizungumza leo Mei 4, 2023 wakati akifungua Mafunzo hayo Mtaalamu wa Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Aneth Moshi amesema mafunzo hayo yatawawezesha Wadau hao kutunza misitu ili kufanya shughuli za uhifadhi na ufugaji nyuki kiuchumi.
‘’ Lengo kuu la sisi kuja hapa ni kutoa elimu endelevu kwa wadau wa sekta za misitu na ufugaji nyuki juu sera za Misitu na nyuki,sheria, kanuni na Miongozo mbalimbali itakayowasadia katika utekelezaji wa majukumu yao na hatimae kufanya sekta hizi kusonga mbele .’’ amesema Moshi.
Naye, Afisa Sheria kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel M.Mganga amesema,rasilimali ya misitu na nyuki ni rasilimali ya watanzania wote ambayo imekasimiwa kwa mujibu wa Sheria kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo inabidi itumike kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo hivyo kupitia mafunzo haya wananchi na wadau muhimu wa sekta ya misitu na nyuki watanufaika kwa kupata uelewa wa Sera na Sheria zinazosimamia sekta hizi muhimu na hivyo kurahisha shughuli za kila siku zinazohusiana na sekta hizi mbili.
"Sheria ya misitu kifungu cha 49 kinaweka masharti ya kuwa na vibali ikiwemo vya uvunaji, usafirishaji na vingine.Ufahamu wa Sheria zinazosimamia sekta hizi ni suala ambalo wakazi wa eneo hili wakifahamu itawasaidia kwa kiasi kikubwa."amesema.
Halima Mchinja akizungumza kwa niaba ya Wanufaika wa mafunzo hayo ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo ambayo yamesaidia kuwapa uelewa kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya misitu na nyuki.
Social Plugin