Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (SMT) Dkt. Angelline Mabula akiongoza hafla ya utiaji saini makubaliano baina ya Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi (SMZ) leo (Mei 20, 2023) jijini Dodoma. Makatibu Wakuu wa Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT), Mhandisi, Anthony Sanga na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi (SMZ), Dkt. Mngereza Mzee Miraji wakitiliana saini makubaliano baina ya Wizara mbili hizo za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hafla ya Utiaji saini baina ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano za Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi (SMZ). Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah Hamad na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ally Saidi wakipeana mikono baada ya kutiliana saini makubaliano hayo katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.
Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi (SMZ) leo (Mei 20, 2023) zimetiliana saini hati za Makubaliano yatakayoziwezesha Wizara hizo zisizokuwa za Muungano kutatua changamoto zinazozikabili katika kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa SMT, Dkt. Angelline Mabula akizungumza katika hafla hiyo ya makubaliano Jijini Dodoma amesema kuwa sekta ya ardhi ya nyumba ni sekta ambayo ni muhimu katika kuwaletea wananchi maisha bora.
"Hatuwezi kuwa na maisha bora kama mipango yetu haijakaa vizuri na hatuwezi kuwa na maisha bora kama watu wetu wana migogoro. Hatuwezi kuwa na maisha bora kama hatuwezi kutoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza na pia hatuwezi kama Wizara na sekta zingine zinazotutegemea sisi tutashindwa kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo tuna imani tutajifunza kutoka pande zote mbili, tuweze kuona tutafanyaje,'amesema.
Amesema Wizara ina imani kuwa Zanzibar kuna mazuri waliyoyafanya na Zanzibar watajifunza kwa yaliyofanyika bara yatakayoboresha namna ya kuwahudumia wananchi wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati huo huo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi (SMZ), Rahma Kassim Ali amesema kuwa makubaliano waliyoyaingia baina yao ni vyema ukawekwa mpango kazi na kwamba kasoro yoyote ikijitokeza wakae watatue kwasababu lengo ni kuleta mafanikio.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Hamad Abdallah amesema kwa Shirika sasa ni utekelezaji kama ilivyozungumza Waziri na kwamba tayari Shirika limeshachukua baadhi ya mambo mazuri yanayofanywa na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) kama vile upangishaji wa muda mrefu wa hadi miaka 30 ambayo utekelezaji wake umeaanza kwa kuwekwa katika maandiko tayari kwa utekelezaji.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar, Mwanaisha Ally Saidi amesema kuwa katika makubaliano hayo wamekubaliana mambo mengi, lakini kubwa ni kubadilishana wataalamu hasa upande wa Zanzibar hawana baadhi ya Wataalamu kwa kuwa NHC lilianza muda mrefu na lina uzoefu mkubwa.
Kwa Upande wa ngazi ya Wizara Makatibu Wakuu wa Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT), Mhandisi, Anthony Sanga na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi (SMZ), Dkt. Mngereza Mzee Miraji walitiliana saini makubaliano baina ya Wizara mbili hizo za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwenye ngazi ya Mashirika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Hamad Abdallah Hamad na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar Mwanaisha Ally Saidi wametiliana saini mkataba huo katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.
Kuhusu Makubaliano hayo mapya ya ushirikiano yatakayodumu kwa miaka kumi kuanzia tarehe yaliyosainiwa yatawezesha taasisi hizo kuweka mipango ya kubadilishana mawazo na ujuzi na kuweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa Watanzania wengi, hususani vijana katika kupata ujuzi wa kuutumia kwenye kuongeza tija kwenye sekta ya ujenzi nchini.
Eneo jingine ambalo ni muhimu katika mustakabali wa taasisi hizi ni rasilimali watu na mbinu bora ili kuwezesha kuhamisha utaalamu, ujuzi na kujengeana uwezo kwa faida ya pande zote mbili hivyo kuwaongezea umahiri pamoja na maarifa zaidi na utamaduni wa mazingira ya kazi husika
Makubaliano hayo pia yataziwezesha taasisi hizo mbili kuainisha fursa za mafunzo na kushirikiana kupeana nyenzo za mafunzo na kubadilishana taarifa muhimu zinazohusu uendeshaji wa mashirika yao bila kuathiri sera zinazolinda usiri wa taasisi hizo.
Katika makubaliano hayo, wataalamu wa maendeleo ya biashara na utafiti wa Shirika la Nyumba la Zanzibar watafaidika kupatiwa mafunzo kwa mujibu wa taaluma zao kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.
Ushirikiano wa Shirika la Nyumba la Taifa na Shirika la Nyumba la Zanzibar upo kwa muda mrefu lakini Mkataba mpya wa ushiririkiano wa sasa utatoa fursa kubwa zaidi kuhakikisha Maendeleo ya pande zote mbili yaliyofikiwa na Mashirika hayo yanawanufaisha wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Mashirika la NHC na ZHC yamesainiana mkataba huo baada ya kutambua mahitaji ya kuongeza mashirikiano kati yao yenye lengo la kustawisha mabadilishano ya ujuzi na welewa mpana kati ya pande mbili hizo na kufikia malengo yao kwa haraka na tija.
Social Plugin