Na Dotto Kwilasa, DODOMA.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa minara ya simu vijijini kati ya serikali na watoa huduma ambao ni kampuni za Airtel Tanzania, TTCL, Vodacom Tanzania, Mic Tanzania (Tigo) na Vietel (Halotel).
Akiongea leo Mei 13, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla hiyo Rais Samia amesema
Benki ya Dunia imeendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya mawasiliano, ambapo inagharimu Dola za marekani milioni 50 katika Mradi wa Kidijitali .
Amesema mradi huo utasaidia zaidi ya minara 1000 kujengwa na kuongezwa nguvu katika maeneo ya vijijini ambapo itasaidiana na sekta binafsi kuongeza ufanisi wa mtandao kwa watanzania takriban milioni 3 kuifikia kasi ya 4G, mradi pia utaunganisha Wizara zote na taasisi zote za Serikali katika mtandao wa kasi ya juu.
Amesema huduma hizo za mawasiliano zinakwenda kuimarisha huduma za matibabu kimtandao vijijini, hivyo itarahisisha utoaji wa huduma hizo kwa wananchi wa pembezoni.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Mhandisi Peter Ulanga amesema Serikali kupitia Shirika hilo inatarajia kujenga minara 54 kwenye Kata 104 maeneo ya vijijini huku wakiendeleza kutoa huduma hiyo kwa Kata 130 na kueleza kuwa huduma hiyo itaboresha mawasiliano na kuwa kichocheo kiuchumi.
Amesema katika minara hiyo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) walishinda zabuni katika kata 104 na watajenga minara 104, Vodacom Tanzania amelishinda kata 190 watajenga minara 190, Airtel Tanzania walishinda kata 161 na watajenga minara 168 , Tigo walishinda zabuni katika kata 244 na watajenga minara 262 na Haloteli walishinda zabuni katika kata 34 na watajenga minara 34.
Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema katika kuhakikisha wanafikisha huduma ya mawasiliano vijijini wanaenda kujenga minara 758 katika kata 713.
Amesema katika mkataba huo wanaenda kuongea nguvu katika minara 304 ambayo ilikuwa inatoa huduma ya 2G sasa itaanza kutoa huduma kwa 3G na maeneo mengine 4G.
“Lengo kubwa la kuanzisha UCSAF ni kupeleka mawasiliano maeneo ya vijijini na kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya mawasiliano bila vikwazo ambapo katika kuhakikisha hilo hadi sasa tumeshajenga minara nchi nzima .
Ameongeza kuwa :”USCAF Imepeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma ambapo hadi sasa tumepeleka katika shule 4750.pia tunaendelea na mradi wa tiba mtandao lengo ni kuhakikisha watanzania wanapata huduma bila kwenda Hospitali.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ameahidi kutoa kompyuta 50 kwa serikali lengo kuongeza chachu ya mafunzo kwa kutumia TEHAMA shuleni.
Chongolo amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kuturahisihsia mambo na kuongeza chachu ya maendeleo.
“Kwa tukio hili muhimu la utiaji saini ujenzi wa minara ya mawasiliao kwa niaba ya CCM tunaipongeza serikali kwa kuchukua uamuzi wa msingi ambao unaenda kutekeleza ilani ya uchaguzi ya 2020/2025 kwa kiwango kikubwa.
Social Plugin