Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Uhusiano wa TEA alipotembelea banda la TEA katika kilele cha maonesho ya Elimu ya Ufundi Jijini Arusha
NA EMMANUEL MBATILO
*******************
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuendelea kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi kupitia programu za Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi ambayo yanatolewa kupitia vyuo na taasisi mbalimbali za Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi nchini.
Katambi ametoa kauli hiyo alipokuwa akifunga Maonesho ya pili ya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi yaliyoanza Mei 16 hadi 22, 2023 Jijini Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid yakiwa na kauli mbiu isemayo, “Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Nguvukazi Mahiri”
Akiwa ndani ya uwanja huo, Katambi alitembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania ambayo imeshiriki kupitia Mafunzo ya Ujuzi yanayotolewa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia, na kukutana na baadhi ya wanufaika walioshiriki wakiwa na bidhaa zao.
“Binafsi najua kazi inayofanywa na TEA na mimi ni balozi wao kwa kazi nzuri maana nimeshuhudia jinsi vijana wanavyonufaika na fursa hizo za mafunzo hivyo nawapongeza sana na naomba wazidi kushirikiana na Idara za Serikali, wadau na makampuni mengine yanayotoa mafunzo ya ujuzi kama wao ili kuwafikia vijana wengi zaidi kwa wakati mmoja, amesema Katambi”
Amesema, amefurahishwa kuona jinsi wadau wa Elimu ikiwemo TEA wanavyoshirikiana na vyuo mbalimbali kukuza ujuzi na huduma bora na kutoa rai kwa wadau hao kuendeleza ushikiano huo ili kuhakikisha kuwa wanapata nguvukazi inayokidhi mahitaji ya soko la ajira hapa nchini.
Aidha, amewata vijana kutumia fursa zinazotolewa kupitia Elimu ya Ufundi na Mafuzo Stadi kama nyenzo ya kutataua changamoto za kiuchumi zinazowakabili ili waweze kujikwamua na kujitengenezea kipato kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali za kibiashara.
Amesema, Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi inaweza kuwa mkombozi wa changamoto ya ajira kwa vijana lakini ni lazima wazingatie na kutekeleza kwa ufanisi yale wanayofindishwa kwa nadharia na vitendo. Kijana asipojitambua na asipotekeleza wajibu wake fursa nyingi zitampita na atabaki kuwa na changamoto siku zote.
“Naomba nitoe rai kwa vijana kutumia fursa wanazozipata kwa umakini ili wawe na mafanikio chanya kwa kujiajiri, kuajiriwa ama kuajiri wengine na kuchangia kukua kwa uchumi wa Taifa" amesema Katambi.
Bi. Eunice Kavishe, mnufaika wa Mafunzo ya Ujuzi akitoa huduma ya Ufundi Simu ndani ya banda la TEA wakati wa kilele cha maonesho ya Elimu ya Ufundi Jijini Arusha
Social Plugin