Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ametaja mikakati ya serikali ya kuwawezesha vijana wa Skauti nchini ikiwamo mafunzo ya fani kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini.
Katambi ameyasema hayo Mei 17, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mhe. Asha Abdullah Juma.
Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji mkakati wa serikali wa kuwawezesha kimaendeleo vijana wa skauti nchini.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Katambi amesema kama ilivyo kwa vijana wengine wote wa Tanzania wakiwamo vijana wa skauti ambao wapo kati ya miaka 15 hadi 35, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania imeendelea kutekeleza program mbalimbali.
Amesema program hizo ni pamoja na klabu za skauti katika shule za msingi na sekondari ambapo vijana hupatiwa mafunzo ya ujasiri, kutatua matatizo katika jamii, kujitolea na uzalendo.
Vilevile, amesema vijana wa skauti ni miongoni mwa vijana ambao hunufaika na programu mbalimbali zinazosimamiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na fursa za mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha miradi ya uzalishaji mali inayowawezesha kujiajiri pamoja na mafunzo ya fani mbalimbali kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini.
Social Plugin