Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHENGERWA AWAASA WANANCHI KUTOSHIRIKI UHALIFU, AWAPONGEZA ASKARI WA UHIFADHI WA MANYARA KUZINGATIA WELEDI


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaasa wananchi kuacha tabia ya kuwashambulia Askari wa Uhifadhi pindi wanapokamata wahalifu huku akiwapongeza Askari wa Uhifadhi wa Manyara kwa kuzingatia maelekezo aliyoyatoa kwa askari wote wa uhifadhi nchi nzima ya kuwataka kutumia busara , weledi na kuzingatia sheria wakiwa kwenye doria badala ya kutumia nguvu zisizohitajika.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2023 wakati alipoongea na Vyombo vya Habari kuhusu tukio la uvamizi wa majangili katika eneo la Hifadhi la Ziwa Manyara waliokamatwa na Askari wa uhifadhi bila kutumia nguvu wala silaha ambapo baada ya kukamatwa wakiwa ndani ya ziwa hilo, majangili walio karibu na boti ya doria waliwasaidia watuhumiwa na kutaka kuzamisha boti hiyo.

Amesema baada ya purukushani hiyo majangili wenzao wapatao 40 waliokuwa karibu na tukio walikuja na kuanza kuwashambulia Askari wanne waliokuwa kwenye boti na kuharibu mashine ambapo askari hao walijipa ujasiri wakapiga makasia na hatimaye kutia nanga katika eneo la Nyati.

Ameongeza kuwa baada ya kuweka nanga katika eneo la Nyati, eneo ambalo askari mmoja wa uhifadhi aliuawa kwa kushambuliwa na Nyati katika siku za hivi karibuni, majangili hao waliendelea kuwashambulia lakini askari hao waliendelea kutumia busara na hawakuweza kutumia silaha walizonazo.“Kwa kuwa nilishatoa maelekezo kwa askari wote wa uhifadhi nchi nzima kutotumia nguvu wakati wa ukamataji wahalifu hata inapokuwa ndani ya hifadhi, watumie busara na weledi na pamoja kwamba askari hawa walikuwa na silaha hawakutumia nguvu wala silaha hali hii ilipelekea majangili hao kushirikiana na wenzao kuwavamia na kuwateka askari na wale watuhumiwa ambao walikuwa wamekamatwa na kutiwa pingu.” Amefafanua

Ameeleza kuwa majangili hao walifanikiwa kuwatorosha watuhumiwa wakiwa chini ya ulinzi na wakiwa na pingu ambapo askari wa uhifadhi waliomba msaada mara moja kwa askari wenzao na wakatoa taarifa kwa jeshi la polisi na polisi walipofika walifanikiwa kuwaokoa askari wa uhifadhi waliokuwa wakishambuliwa na kutaka kuuawa na majangili hao.

Amesema baada ya tukio hilo majangili walikusanyika tena na kuanza kuvamia kwenye Ofisi ya vijiji na kutaka kuingia kwenye lango la Ofisi za Hifadhi ya Manyara ambapo amesema Jeshi la Polisi walitumia takribani masaa manne kuzuia vurugu hizo ili wasiingie ndani ya Hifadhi kufanya uhalibifu au matukio mengine ya kiuhalifu ambapo pia walitumia mabomu ya machozi.

Amesema hata baada ya kutumia mabomu ya machozi bado vurugu ziliendelea na kupelekea mtu moja kufariki.

Akisimulia kwa uchungu Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa tukio hilo ni la kusikitisha kwa kuwa haya yote yasingeweza kutokea kama wananchi wangetii sheria, aidha askari wote wa hifadhi wangeweza kuzama kwenye maji baada ya kushambuliwa na majangili na wananchi kuanza kuchukua sheria mkononi kwa kuwashambulia wahifadhi bila kuogopa na kuwatorosha watuhumiwa waliokamatwa kwa kufuata taratibu bila kuwapiga wala kutumia silaha walizokuwa nazo.

Amesema Serikali imeandaa maeneo mengi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za uhifadhi, kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo wananchi wangeweza kuyatumia kwa kuzingatia sheria ambazo zimetungwa na wawakilishi wao bungeni kwa miaka mingi kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye badala ya kuwa sehemu ya uhalifu.
“Sisi kama Serikali tunatamani kuona kila mwananchi awe na furaha lakini tunawaomba watanzania, hatupaswi kugombana kwa kuwa maeneo ni mengi, naomba sana wananchi wafuate sheria, iwapo kila mtanzania akitii sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe hakutakuwa na mivutano yoyote baina ya wananchi na wahifadhi, na sisis tumejitahidi katika kipindi hiki kifupi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu, tunaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kuwa wananchi ndiyo wahifadhi namba moja” Amesisitiza

Aidha amewataka wahalifu wote walioshiriki katika tukio hili kujitokeza mara moja kwenye jeshi la polisi kwa kuwa tayari taarifa ilifatolewa kabla ya tukio hilo kuwa kubwa ambapo amelishukuru jeshi la polisi kwa kuokoa askari wa uhifadhi ambao ni watoto wa watanzania ambao wanafanya kazi kubwa ya uhifadhi wa raslimali kwa faida ya taifa zima.

Kufuatia vurugu hizo Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu 12 wanaodaiwa kufanya uhalifu na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka vinara wa vurugu hizo ambapo pia amesisitiza kwa wananchi kuzingatia sheria za nchi na kuacha tabia za uvuvi haramu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com