Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amekutana na kufanya vikao na wananchi wa vijiji vyenye migogoro ya mipaka na Hifadhi ya Serengeti na kuutaka uongozi wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kuimarisha program za ujirani mwema na kuwashirikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wakati wa kupanga mipango yao ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa raslimali hizo na kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Mei 28, 2023 wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tarime na kufanya mikutano kwenye vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi ya Serengeti vilivyokuwa na migogoro na mipaka katika zoezi la uwekaji wa vigingi vya mipaka ambapo wananchi wa maeneo hao wamepongeza kwa hatua hiyo ya Serikali ya kuja na kuwasikiliza na kuahidi kushirikiana na Serikali kwenye uhifadhi.
Mhe. Mchengerwa aliambatana Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yake Anderson Mutatembwa na Kamishna wa TANAPA, Afande William Mwakilema na kupokewa na uongozi wa Mkoa wa Mara, uongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime na Mbunge wa Tarime vijijini Mhe. Mwita Waitara ambapo katika mikutano hiyo yote Mhe. Mchengerwa aliongoza vikao hivyo kwa kuwapa wasaa wa wananchi kutoa maoni na mawazo yao na mwisho alitolea ufafanuzi wa hoja hizo na nyingine kuzichukua kwa hatua zaidi.
Wananchi wamepongeza hatua hiyo ya Waziri Mchengerwa kwenda na kuwasikiliza huku wakieleza kuwa kumekuwa na ushirikishwaji mdogo na kuiomba Serikali kupanga kwa pamoja ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Diwani wa kata ya Nyanungu Tiboche Richard amesema kuwa wananchi wa Kata yake wapo tayari kushirikiana na Serikali kwenye kila jambo endapo watashirikishwa na hifadhi.
“Mhe. Waziri napenda kukuhakikishia kuwa leo unatufanya tulale usingizi maana umetumwa na Mhe. Rais wetu kuja kutujengea mahusiano mazuri, na sisi hiki ndicho tulichokuwa tunakikosa.” Amesisitiza diwani Richard
Akiwa kwenye mkutano katika Kijiji cha Karakatonga wilayani Tarime, Mhe. Mchengerwa ameutaka uongozi wa TANAPA kushuka chini kwa wananchi na kwenda kuzungumza nao kwa kuwa hifadhi hizo ni za wananchi na wananchi ndiyo wahifadhi namba moja.
Aidha, amesema wazo la uhifadhi wa raslimali katika taifa la Tanzania limeasisiwa miaka mingi ambapo uongozi katika awamu zote toka enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais Samia Suluhu Hassan limezingatiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Akiwa kwenye Kijiji cha Kegonga, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi hao kushirikiana na uongozi wa Serikali wakati wote na kuacha tabia za kugomea kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanachochea migogoro.
“Kwa hiyo wanapokuja viongozi wa Serikali kuja kujadili mpango wa matumizi bora ya ardhi wasikilizeni msikatae kusikiliza, shaurini tufanye nini.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amewataka kutambua kuwa wahifadhi ni sehemu ya jamii yao kwa kuwa baadhi ya watumishi hao ni sehemu ya familia zao na watoto wao.
Social Plugin