Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Ubora, Ufuatiliaji na Tathmini Dkt. Joyfrey Oleke kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) leo tarehe 9 Mei,2023, Jijini Dodoma, amefungua Mkutano wa Tathmini ya Udahili kwa Wakuu wa Vyuo na Maafisa Udahili wa Vyuo vya Afya.
Dkt. Oleke amesema kikao hicho kimelenga kutoa taarifa ya Udahili wa wanafunzi kwa mwaka masomo 2022/2023 na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha Mfumo wa Udahili wa Pamoja(CAS) kwa kozi za Afya.
Ameongeza kuwa wakuu wa vyuo na maafisa udahili wana mchango mkubwa katika kupunguza changamoto za wanafunzi kwa kuwapa miongozo na taarifa sahihi wakati wa udahili na kufafanua kuwa NACTVET imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na vyuo vya afya hasa wanapokutana na changamoto za kimfumo na taratibu nyingine za uendeshaji wa zoezi la udahili.
Aidha washiriki wa mkutano huo takribani 300 wamepata fursa ya kujadili masuala ya udahili na kupata suluhu juu ya changamoto mbalimbali za kupata ufafanuzi wa namna bora ya kutekeleza majukumu yao.
Mfumo wa CAS umekuwa na faida kubwa ikiwa ni Pamoja na kupunguza gharama za wanafunzi kuomba nafasi za udahili vyuoni.
Washiriki wengine wa mkutano huu kutoka NACTVET ni wakuu wa vitengo mbalimbali akiwepo Bw. Twaha Twaha, Bi. Amina Azizi, Mhandisi Vicent Maro, Dkt. Hirst Ndisa pamoja na wakuu wa kanda.