Kamati ya siasa ya wilaya ya Chamwino ikiongozwa na katibu ndugu Sylivester Yaledi (Chief Yaledi) imetembelea mradi wa Bwawa la maji Membe lililopo kata ya Membe halmashauri ya Chamwino kukagua hatua ya utekelezaji mradi huo.
Kamati hiyo imeipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji NIRC kwa usimamizi makini wa ujenzi wa bwawa la maji Membe litakaloweze kumwagilia zaidi ya hekari 8,000 katika mashamba ya wakulima wa eneo hilo ikiwa ni miongoni mwa miradi ya Umwagiliaji inayoendelea kutekelezwa na tume.
Akielezea maendeleo ya mradi huo msimamizi wa mradi wa ujenzi bwawa hilo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Saleh Madebe (mwenye T-shirt ya njano kwenye picha) amesema mradi huo umefikia asilimia 45.83%.
Hata hivyo kamati hiyo imemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi wa bwawa hilo ili kuendana na muda wa mkataba na hatimaye mradi huo uwe na tija kwa wakulima na kuchochea uchumi wa nchi.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba 1, 2023 kwa mujibu wa mkataba ambapo matokeo ya kukamilika kwa mradi huo utawezesha halmashauri ya wilaya ya Chamwino na mkoa wa Dodoma kuwa na chakula cha kutosha na kuzalisha ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo.