Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi Bwawa la Kidunda litakalojengwa Mkoani Morogoro na kugharimu Tsh Bilioni 335 na litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji kwa yatakayotumika kwa miaka mitatu mfululizo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Morogoro, Kaimu Afisa Mtendaji DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema lengo la utekelezaji mradi huo ni kuwezesha mitambo ya maji ya Ruvu juu na Ruvu chini kuwa na maji ya kutosha ili kuzalisha maji kipindi cha kiangazi.
Aidha Kingu amebainisha kuwa bwawa hilo litakapokamilika litakuwa lina hifadhi maji kipindi cha masika ili maji hayo yaweze kutumika nyakati za kiangazi.
Mbali na upatikanaji wa maji kwa uhakika, Ndugu Kiula ameeleza faida za mradi huo na namna utakavyotoa fursa mbalimbali kwa Taifa ikiwemo Ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 101, uzalishaji wa umeme megawatt 20, uvuvi na utalii ambavyo kwa pamoja vitawanufaisha Wananchi kwa maeneo husika kwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Ujenzi wa mradi wa bwawa la Kidunda utaenda kuleta Uhakika wa upatikanaji wa maji kwa muda wote kwa mwaka mzima lakini pia Kuzalisha umeme katika bwawa la kidunda wa Megawati 20 zitakazoenda kuingia katika Gridi ya taifa pamoja na Kutunza hali ya mazingira kwa viumbe hai.” Aliongeza
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Isalama ya Wilaya ya Morogoro Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Rebeca Msemwa ameipongeza Serikali kwa udhubutu wa utekelezaji wa mradi na kutoa wito kwa DAWASA kuusimamia na kuutekeleza mradi kwa ukamilifu ili ulete manufaa kwa Watanzania.
“Tunajivunia utekelezaji wa mradi huu katika Mkoa wetu wa Morogoro, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha kiangazi hivyo hatuna budi kuunga juhudi hizi kwa kuhakikisha DAWASA wanatekeleza mradi huu kwa ukamilifu kama ilivyo matarajio ya Watanzania “. Alisisitiza
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi ameeleza mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vyanzo vyote vinavyoingia katika bwawa la Kidunda linakuwa na maji ya kutosha kwa kuzuia shughuli zote za uharibifu zinazosababishwa na binadamu au mabadiliko ya tabia ya nchi.
"Tumejipanga kufanya uthamini na tathmini katika maeneo yote yanayozunguka chanzo cha mto Ruvu na kutangazwa kuwa maeneo ya uhifadhi kwa kutenga shilingi Bilioni Nne ili kuhakikisha bwawa la Kidunda linatoa suluhu ya upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani". Alisema Mhandisi Mmasi
Mradi wa Bwawa la Kidunda unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) unatarajia kuanza rasmi Juni 18, 2023 kwa kipindi cha miaka mitatu huku likitarajiwa kupunguza changamoto za huduma za maji kwa Wakazi wa Mikoa ya Dar es salaam na Pwani.
Social Plugin